1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Wa Trump na Putin ulikuwa mkutano hatari

17 Julai 2018

Rais wa Marekani analaumiwa kuonesha udhaifu mkubwa kwenye mkutano na mwenzake wa Urusi mjini Helsinki, kitu ambacho Bernd Riegert anakiita "kosa la kidiplomasia" kwenye jukwaa la kimataifa.

Finnland Helsinki Trump-Putin Treffen | Handschlag
Picha: picture-alliance/Sputnik/S. Guneev

Donald Trump ni rais mzuri, lakini kwa Urusi. Sio kwa Marekani wala si kwa sehemu nyengine za dunia. Wizara ya Mambo ya Nje ilibonyeza "Like" kuonesha kuupenda ujumbe wa Trump kwenye mtandao wa Twitter na hivyo kuepuka kuweka maoni yake moja kwa moja kwenye kauli ya Trump, ambapo aliukosoa "upumbavu na ujuha" wa Marekani kuwa sababu ya mahusiano mabaya kati ya nchi yake na Urusi. 

Hivi kweli ni Marekani ndiyo ya kulaumiwa kwa udukuzi wa Urusi kwenye uchaguzi wa rais wa mwaka 2016, au kwa uamuzi wa Putin kuinyakuwa Crimea? Hiki ni kituko kikubwa na hakikutarajiwa kutokea kwenye historia ya hivi karibuni ya Marekani. Lakini Trump akairejelea tena fikra hii hii kwenye mkutano wake wa kilele na Putin mjini Helsinki hapo jana na, kwa kufanya hivyo, akajishusha mwenyewe hadhi.

Rais wa Marekani hajawahi kuwa kama hivi huko nyuma, na wala hakupaswa kuwa. Lakini swali ni hili: Hadi lini wana-Republican wataendelea kukiunga mkono kichwamchungwa hiki kisicho maarifa kusalia kwenye Ikulu ya White House?

Na Bernd Riegert

Mara kadhaa, Trump hutamka maneno yenye kugongana, nusu ukweli,  nusu uongo. Miongoni mwa ya karibuni kabisa ni mahusiano ya mapenzi na chuki kati ya Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, hoja kwamba Uingereza inapaswa kuushitaki Umoja wa Ulaya kutokana na kura ya kujiondoa, Brexit, kauli tata juu ya mahusiano yake ya Waziri Mkuu Theresa May, na kuiita Ujerumani kuwa ni mfungwa wa Putin lakini baadaye kumuita kiongozi huyo wa Urusi kuwa ni mshindani muadilifu.

Kauli za mtangazaji huyu wa kipindi cha televisheni aliyegeuka kuwa rais zimekuwa ngumu mno kuzisikiliza. Kinyume na Putin, Trump alionekana dhaifu, asiye na uhakika na asiye na matayarisho kwenye mkutano ule wa jana.

Trump hana uwezo?

Wakati wowote Trump anapokiuka taratibu za kidiplomasia, wasaidizi wake hulazimika kukusanya vipande vipande vya kauli za kutatanisha na kuzigeuza kuwa sera inayofahamika. Hadi lini wanataka kuendelea kufanya hivyo?

Kwa Putin, mkutano huu na Trump ulikuwa mtelezo tu. Kikubwa alichotakiwa kufanya ni kukaa na kumsikiliza rais wa Marekani akiuvunjavunja utaratibu wa kidunia.

Ndani ya wiki chache tu zilizopita, Trump amewatenga washirika wake wa NATO, ameiraruwa Uingereza na ameuita Umoja wa Ulaya kuwa ni „adui“. Kwa hakika hasa, amempa Putin zaidi ya kile alichokitarajia.

Tuhuma za Urusi kuingilia mambo ya Marekani zimepita bila Urusi kujihisi ina dhamana ya kubeba. Je, Putin alijaribu kubadili mwelekeo wa uchaguzi wa 2016? Je, alimtaka Trump kuingia madarakani? Je, mikononi mwake ana taarifa nyeti kabisa kumuhusu Rais Trump na familia yake?

Ukiyaweka masuali yote haya pamoja, unaweza kukisia kuwa huo ndio uhalisia, maana lazima kutakuwa na jambo ambalo linamfanya Trump awe kama alivyo mbele ya rais huyo wa Urusi.

Huenda hii ndio sababu Trump akataka kuketi chini na mwenzake wa Urusi mjini Helsinki. Mtu mwenye kiburi asiye na utaalamu anakutana na afisa wa zamani wa ujasusi.

Kitu pekee kinachowaunganisha wawili hawa ni kwamba hawajali kabisa kuhusu ukweli. Putin ameweka wazi kwamba hajali chochote kuhusu imani, bali anaamini kwenye kuyatimiza matakwa yake. 

Hapana shaka ni jambo zuri pale wanaume wawili wenye nguvu wanapozungumza. Lakini onesho hili safari hii limedhihirisha kuwa hiki hakitoshi. Dunia inatarajia kikubwa zaidi, kitu ambacho hata Trump alipaswa kukitambua.

Bahati mbaya, matarajio hayo hayakutimizwa. Bahati mbaya zaidi kwa raia wa Marekani, wana mtu mmoja wa hatari sana na asiyetabirika kwenye ofisi yao ya rais.

Tuombe Mungu asije akasababisha balaa zaidi ya hili ambalo tayari ameshalisababisha.

Mwandishi: Bernd Riegert/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW