Maoni ya Andrea Schmidt juu ya uchaguzi wa Tanzania
5 Novemba 2010Matokeo ya uchaguzi nchini Tanzania yametangazwa rasmi.Chama tawala CCM cha Rais aliemo madarakani,Jakaya Kikwete kwa mara nyingine kimeshinda kwa kura nyingi. Jee sasa mambo yataendelea vilevile au vyama vya upinzani vitaweza kuwa na sauti mbele ya utawala ulioota kutu wa chama tawala.?
Watanzania wameshaamua.Wamemchagua Jakaya Kikwete kwa kipindi kingine cha miaka mitano na cha mwisho. Chama chake cha Mapinduzi CCM,kimekuwamo madarakani tokea Tanzania ijipatie uhuru. Kwa mara ya kwanza safari hii chama hicho kilikabiliwa na ushindani mkali katika uchaguzi. Katika maeneo fulani vyama vikuu vya upinzani vilifanikiwa kupata kura nyingi kuliko CCM. Vyama 18 vilishiriki katika uchaguzi huo.
Kwa mara ya kwanza tokea kuanzishwa mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1992 nchini Tanzania uchaguzi huo ulikuwa wa kusisimua, kwa Watanzania wenyewe na kwa jumuiya ya kimataifa.
Ulikuwa wa kusisimia hasa kutokana na mgombea wa chama cha upinzani Chadema Wilbrod Slaa .Kwa kutumia kigezo cha rais Obama ,Slaa ambae hapo awali alikuwa kasisi alitoa mwito wa kuleta mabadiliko katika siasa za nchi na mpaka dakika ya mwisho alitoa changamoto. Miongoni mwa wanaomuunga mkono ni wapiga kura vijana wanaotaka kuona mabadiliko katika uongozi.
Katika faharasi mpya juu ya viwango vya maisha Tanzania ipo nyuma, katika nafasi ya 148 kati ya nchi 169. Pia kutokana na mazingira hayo yapasa kuuliza swali: vipi imewezekana kwa chama tawala CCM kuchaguliwa tena kwa kura nyingi,ingawa chama hicho kwa kiwango kikubwa hakikuzitekeleza ahadi zake juu ya kupambana na rushwa na kupunguza umasikini.?
Kutokana na kucheleweshwa kutangazwa matokeo, palizuka mashaka, na mpinzani mkuu Slaa alitaka kura zihesabiwe tena.
Sababu ya ushindi wa CCM inaweza kuwa ni kwa vile inazo nyenzo nyingi na hasa watu wazima ambao ni watiifu wa chama.Pamoja na hayo vyama vya upinzani ni dhaifu na vimegawanyika.Chama cha CCM pia kinanufaika na jina la Mwalimu Nyerere mwasisi wa taifa la watanzania na sifa zake - uwezo aliokuwa nao wa kuona mbali na uadilifu wa kutokuwa na makuu. Lakini chama CCM, licha ya ushindi wake mwingine, kimo njiani kuupoteza urithi huo
Wapiga kura wengi hawapo tayari kukubali tofauti kubwa iliyopo baina ya viongozi wa CCM waliojaza mifuko,na wananchi wengi kapuku. Lakini mabadiliko ya dhati ya yametokea kisiwani Zanzibar,ikiwa ni matokeo ya kura ya maoni ya mwezi juni yaliowawezesha wapinzani kushiriki katika mchakato wa demokrasia. Hatahivyo licha ya kupoteza wapiga kura, CCM imeweza kutetea wingi wake ,lakini uso wake umeonyesha alama za masumbwi!
Mwandishi:Schmidt Andrea/Afrika-Kiswahili
Tafsiri:Mtullya Abdu
Mhariri:Josephat Charo