1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Italia

Abdu Said Mtullya26 Februari 2013

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni juu ya uchaguzi mkuu wa nchini Italia.Wote wanatilia maanani kurejea ulingoni kwa Berlusconi

Mjumbe wa chama cha Democratic Pier Luigi Bersani,akipiga kura
Mjumbe wa chama cha Democratic Pier Luigi Bersani akipiga kuraPicha: Alberto Lingria/AFP/Getty Images

Mhariri wa gazeti la "Mannheimmer Morgen" anasema jambo zuri juu ya matokeo ya uchaguzi wa nchini Italia ni kwamba Silvio Berlusconi hakushinda! Hata hivyo mhariri huyo anasema habari mbaya ni kwamba Berlusconi hakuanguka kabisa. Ndiyo kusema mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Italia mara nne amelifikia lengo lake, yaani kuifanya Italia isitawalike.

Mhariri wa gazeti la "Flensburger Tageblatt"anasema matokeo ya uchaguzi wa nchini Italia ni ishara ya tahadhari. Mhariri huyo anatilia maanani idadi ya kura alizozipata msanii wa uchekeshaji na idadi ya kura alizozipata Silvio Berlusconi.

Anaeleza kuwa Ikiwa robo ya wastahiki katika uchaguzi, na hasa vijana wamempigia kura mtu asiyekuwa na programu yoyote na wala asiyekuwa na tajiriba ya kisiasa, basi pana haja kuwapo tahadhari. Katika upande mwingine yupo Berlusconi aliyepata kura za kumwezesha kuingia katika baraza la seneti. Mwanasiasa huyo atatumia kila fursa kuionyesha misuli yake ya kisiasa katika baraza hilo. Na kwa hivyo hakuna mwenye matumaini ya kuyaona mabadiliko makubwa nchini Italia.

Hulka ya Italia vigumu kutawalika

Mhariri wa gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger"anasema matokeo ya uchaguzi nchini Italia yanaonyesha kwamba nchi hiyo imo katika hatari ya kutumbukia katika hali ya kutoweza kutawalika. Naye mhariri wa "Darmstädter Echo"anasisitiza kuwa Italia ni mbiu ya mgambo katika muktadha wa mgogoro wa Euro. Mhariri huyo anafafanua kwa kusema kwamba haitoshi kutoa lukuki za fedha ili kuiunga mkono mifumo ya fedha, na kuzitaka serikali zinazosaidiwa zifanye mageuzi.

Mshikamano baina ya nchi zenye nguvu na zile dhaifu maana yake pia ni kuchukua hatua za kupambana na hali mbaya inayowakabili watu wengi katika nchi hizo, na hasa maafa ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana. Hivi sasa tunachoshuhudia ni kuzama kwa rika zima la vijana katika nchi za kusini mwa Ulaya.

Tahadhari kwa Ujerumani

Gazeti la"Kieler Nachrichten"linaitahadharisha Ujerumani juu ya matatizo ya kiuchumi yanayoikabili Italia na linasema matokeo ya uchaguzi nchini Italia, kwa mara nyingine yameithibitisha hulka ya nchi hiyo, yaani kuwapo kwa hali ya kutotawalika. Lakini inapasa kuzingatia kwamba, tokea kuanza kwa mgogoro wa Euro, matatizo ya Italia pia yamekuwa matatizo ya Ujerumani. Ikiwa nchi hiyo, ambayo ni ya tatu kwa nguvu za kiuchumi katika Ukanda wa sarafu ya Euro, haitaweza kuondokana na mshuko wa uchumi,athari zake zitaikumba Ujerumani siku moja.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW