Maoni ya wahariri juu ya Krimea
19 Machi 2014Mhariri wa gazeti la "Der neue Tag" anasema Umoja wa Ulaya sasa unapaswa kufikiria njia mpya juu ya jinsi ya kuhusiana na Urusi.Na anasema la muhimu zaidi ni kutafuta njia ya kuondokana na kuitegemea Urusi kwa mahitaji ya nishati.
Utulivu kwa Ukraine
Mhariri wa gazeti la "Lausitzer Rundschau" anazishauri nchi za Umoja wa Ulaya kuweka mkazo zaidi katika kuleta utulivu nchini Ukraine, lakini bila ya kuipa nchi hiyo ahadi nyingi. Mhariri huyo anaeleza kwamba haifai kuendelea kuutumia muda mwingi kwa ajili ya kufikiria juu ya vikwazo zaidi dhidi ya Urusi.Badala yake, sasa inapasa kuangalia jinsi ya kuisaidia Ukraine ili iweze kurejesha utengemavu.Na wakati huo huo litakuwa shauri zuri kuepuka kuipa Ukraine ahadi ya kuiingiza katika Umoja wa Ulaya au katika jumuiya ya ulinzi ya NATO.Lengo linapasa kuwa moja tu sasa;kuiimarisha Ukraine.
Mhariri wa gazeti la "Kieler Nachrichten anasema kinachohitajika sasa ni mkakati wa kidiplomasia ili kuondokana na siasa ya vigongo mkononi baina ya Urusi na nchi za magharibi.Nchi za magharibi zinapaswa kutambua kwamba Urusi haitakubali Ukraine isogee karibu na Nato,kama jinsi ambavyo nchi za magharibi hazitakubali mipaka ya Poland ihujumiwe. Katika muktadha huo,lazima Ukraine iwe na mahala pake huru.
Ni sahihi Ujerumani kuzisaidia nchi nyingine
Mahakama Kuu ya Ujerumani ,imeuthibitisha uhalali wa Ujerumani kushiriki katika mpango wa kuzisaidia nchi zinazokabiliwa na mgogoro wa madeni barani Ulaya.
Gazeti la "Südwest Presse" linasema Ujerumani inayo haki ya kushiriki katika mpango wa kuzisaidia nchi zinazokabiliwa na mgogoro wa madeni.Huo ni uamuzi sahihi. Gazeti hilo linahoji kwamba uamuzi mwingine wowote ungelisababisha hali ya wasiwasi barani Ulaya.
Naye mhariri wa gazeti la "Nordwest" anasema sasa utatanishi umeondoshwa juu ya dhima ya Ujerumani katika mpango wa kuzisaidia nchi nyingine barani Ulaya.Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Ujerumani bila shaka utayatuliza masoko ya fedha barani Ulaya na pia utazuia njama za walanguzi.Wasi wasi ulikuwa mkubwa zaidi juu ya mgogoro wa madeni kuliko juu ya uhalali wa kikatiba.
Mwandishi:Mtullya abdu.Deutsche Zeitungen:
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman