Maoni ya wahariri juu ya Misri na bajeti ya Marekani
28 Desemba 2012Juu ya Misri gazeti la "Westdeutsche" linasema kwa kuipitisha katiba mpya, Misri imepiga hatua ya kwanza kuelekea katika nchi itakayotawaliwa katika msingi wa sheria za kidini. Nchi ambamo haki za raia kwa jumla, na hasa za wanawake zitatimbwa.Lakini sasa itapasa kusubiri na kuona iwapo pande zenye misimamo mikali zitakazoendelea kuwamo madarakani, zitafanikiwa kuwapatia wananchi ajira. Kwani sababu mojawapo ya kuangushwa kwa Mubarak ilikuwa kushidnwa kuyatatua matatizo ya kijamii.
Huenda mwanamke hataruhusiwa tena kupaka rangi ya mdomo, au kutoka nyumbani kwake bila ya kujitanda hijabu, nchini Misri. Hayo ni maoni ya gazeti la "Hessische Niedersächsische Allgemeine"
Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba maandamano yanayofanyika kwenye uwanja wa Tahrir yanaonyesha, ni kwa kiasi gani watu wa Misri wana wasiwasi juu ya katiba mpya. Mhariri huyo anasema na hasa Ibara ya kumi ya katiba hiyo inawatia hofu vijana na Wamisri wengine wasioegemea katika upande wa kidini. Ikiwa dini ndio utakuwa mwongozo wa kuilinda familia, basi hivi punde polisi wa kidini watapiga hodi kwenye nyumba za watu na kuwalazimisha kuvaa hijabu.
Sakata la bajeti,Marekani
Mpaka sasa utawala wa Obama na wabunge wa Republican hawajapatana juu ya kukitegua kitendawili cha bajeti. Na ikiwa hadi mwishoni mwa mwezi huu, halitapatikana suluhisho, basi Marekani itaingia katika mdororo wa uchumi. Gazeti la "Augsburger Allgemeine" linasema kila upande unajaribu kujipatia ushindi dhidi ya upande mwingine. Lakini suala la bajeti ni muhimu sana nchini Marekani.
Uchumi wa nchi hiyo na masoko ya dunia yatayumbishwa.Na kwa hivyo badala ya kuvutana,Repulican na Demokrats wanapaswa kufikia mwafaka. Lazime pawepo nia njema ya kusikilizana.
Mhariri wa "Coburger Tageblatt" pia anatilia maanani kwamba njama za kisiasa zinaendekezwa na pande zote mbili, badala ya kuyajali maslahi ya wananchi wa Marekani. Na gazeti la "Die Welt" linatahadharisha! "Ikiwa suluhisho halitafikiwa baina ya vyama vya Republican na Demokratik, masoko ya hisa yataanguka japo kwa muda mfupi duniani kote.
Hali hiyo itasababisha madhara kwenye mashirika ya pensheni na katika akiba za watu kwenye mabenki.Njia iliyobakia ni kwa Marekani kupunguza matumizi. Lakini Marekani sawa na bara la Ulaya inakabiliwa na tatizo la msingi katika muundo wa bajeti yake.Ugiriki ipo kote duniani:
Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche zeitungen:
Mhariri: Josephat Charo