1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kuleta mkataba wa TTIP mashakani

Admin.WagnerD29 Agosti 2016

Wahariri wanazungumzia juu ya kauli iliyotolewa na Makamu wa Kansela wa Ujerumani, Gabriel kwamba mazungumzo juu ya kuanzisha biashara uhuru baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani,TTIP yameshindikana.

Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Makamu wa Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema Umoja wa Ulaya na Marekani zimeshindwa kufikia makubaliano kwenye mazungumzo ya kuanzisha biashara huru na ya haki, baina yao, mazungumzo ambayo kwa jumla hayaungwi mkono na watu wengi barani Ulaya.

Mhariri wa gazeti la "Nord West" anasema ikiwa bwana Gabriel, ambae pia ni Waziri wa uchumi anaitoa kauli hiyo, huo unaweza kuzingatiwa kuwa msimamo rasmi wa serikali ya Ujerumani.

Mhariri wa gazeti la "Nord West" anasema mazungumzo hayo ya TTIP, ya kuleta mkataba wa kuanzisha biashara huru na ya haki baina ya nchi za Ulaya na Marekani yanapingwa pia na baadhi ya watu katika vyama vikuu vya nchini Ujerumani vya Social Democratik na Christian Democratic Union.

Mhariri huyo pia anatilia maanani kwamba mkataba wa TTIP unatiliwa mashaka pia na idadi kubwa ya wananchi barani Ulaya. Hata hivyo anahoji kwamba mkataba huo ni muhimu kwa Ujerumani.

Lakini mhariri wa gazeti la "Nürnberger Nachrichten" anamuunga mkono Makamu wa Kansela, Sigmar Gabriel juu ya mkataba huo wa biashara huru kwa kueleza kwamba watu wengi hawajaulewa msimamo wa Makamu wa Kansela huyo , Gabriel juu ya mkataba wa biashara huru. Yeye pia ameutambua ukaidi wa Marekani kwenye mazungumzo hayo. Marekani haiko tayari kufikia mwafaka na nchi za Ulaya juu ya jambo lolote.Marekani haiko tayari kuusikiliza upande mwingine.

Majeshi ya Uturuki njiani kuingia katika dafrao na Marekani nchini Syria:

Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linauzungumzia mgogoro wa nchini Syria katika muktadha wa kujiingiza zaidi kwa Uturuki katika mapigano. Mhariri wa gazeti hilo anatahadharisha juu ya hatari ya kutokea mgongano baina ya majeshi ya Uturuki na washauri wa kijeshi wa Marekani kaskazini mwa Syria. Mhariri huyo anaeleza kwamba pana uwezekano wa vikosi maalumu vya Marekani vinavyotoa ushauri wa kijeshi kwa Wakurdi wa kaskazini mwa Syria kupambana na majeshi ya Uturuki.

Vifaru vya Uturuki nchini SyriaPicha: Reuters/U.Bektas

Mhariri anasema Rais Obama anatumai kwamba operesheni ya kijeshi ya Uturuki , itakuwa ya muda mfupi na kwamba italenga shabaha sahihi.

Lakini Marekani inapaswa kutoa mwito kwa Wakurdi wa kuviachia vifaru vya Uturuki viendelee na safari, na wakati huo huo Marekani itapaswa kuwaambia Waturuki wasivuke mipaka.Hata hivyo hakuna mwenye uhakika iwapo miito hiyo itaitikiwa.
Gazeti la "Der Neue Tag " linatoa maoni juu ya mjadala unaohusu kupiga marufuku mavazi ya Burka na Burkini. Mhariri wa gazeti hilo anasema ni sawa kabisa kuwataka watu wazionyeshe nyuso zao, lakini hiyo isiwe sababu ya kuendesha sera ya chuki dhidi ya Uislamu.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Iddi Ssessanga