1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

.

Abdu Said Mtullya7 Januari 2015

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanauzingatia mvutano baina ya India na Pakistan,mgogoro wa wakimbizi barani Ulaya na juhudi za chama cha FDP za kufufuka katika ngazi ya kitaifa

Mwenyekiti wa chama cha Waliberali FDP Christian Lindner
Mwenyekiti wa chama cha Waliberali FDP,Christian LindnerPicha: picture-alliance/dpa/B. Weißbrod

Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linasema ya mvutano baina ya India na Pakistan juu ya jimbo la Kashmir unahitaji cheche ndogo tu ili kuuwasha mtoto mkubwa. Gazeti hilo linasema mvutano umeshtadi baina ya nchi mbili hizo na mapigano yametokea kwenye mpaka wao wa pamoja.

Pakistan na India zinalipigania jimbo la Kashmir. Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linasema, ni cheche ndogo tu inayoweza kuleta maafa makubwa .Gazeti hilo linatilia maanani kwamba uwezekano huo ni mkubwa katika eneo la kusini mwa Asia palipojaa silaha za nyuklia. Mhariri wa gazeti hilo anasema sasa watu wanatumai kwamba busara itazingatiwa katika pande zote mbili.

Naye mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" anasema ili kuutatua mgogoro wa Kashamir pande zote zinazohusika, yaani India na Pakistan zinapaswa kuonyesha dhamira ya kufikia suluhisho. Lakini mhariri huyo anasema hapo ndipo penye tatizo. India na Pakistan zimetingwa na matatizo ya ndani.

Wakimbizi na Umoja wa Ulaya

Gazeti la "die tageszeitung" linauzungumzia mgogoro wa wakimbizi kwa kuiangalia sera ya Umoja wa Ulaya. Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha kwamba lengo la Umoja wa Ulaya ni kuwakomesha matapeli wanaowaingiza watu barani Ulaya kinyume na sheria. Lakini anasema mpaka sasa tunachokiona ni tabaini yake.

Mharirihuyo anaeleza kuwa kwanza inapasa Umoja wa Ulaya ujue kwamba kadri unavyoendelea kujifungia ndani ya mipaka yake, ndivyo biashara ya matapeli inavyozidi kustawi. Na kwa hivyo, ili kuing'oa mizizi ya ustawi huo, Umoja wa Ulaya unapaswa kuianzisha sera itakayoruhusu kuwapokea wakimbizi wanaotoka katika maeneo ya migogoro.

Chama cha FDP kurejea katika siasa za kitaifa
Chama cha waliberali-FDPambacho mnamo miaka ya nyuma kilikuwamo katika serikali kadhaa za Ujerumani sasa kimetoweka katika siasa za kitaifa tokea kishindwe katika uchaguzi wa kuingia bungeni mnamo mwaka wa 2013. Lakini chama hicho kimefanya mkutano wa kujaribu kujifufua kwa kuizindua nembo mpya.

Gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger" linasema nembo mpya pekee haitatosha kukipa chama cha Waliberali fursa ya kuendelea kuwa na maana katika siasa za Ujerumani. Hata hivyo siyo wazo baya kujaribu kujisafisha na kujivalisha nguo mpya.

Lakini mhariri wa gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger" anaeleza kuwa kilichoonekana kwenye mkutano ni ukweli kwamba ni wajumbe wachache tu wanaopendeza wakivaa nguo hizo mpya kama Mwenyekiti wa chama . Ndiyo kusema siasa za mtu mmoja zitaendelea kwa muda kukigubika chama cha Waliberali-FDP.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW