1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Snowden

Abdu Said Mtullya3 Julai 2013

Mkasa wa aliekuwa wakala wa shirika la ujasusi la Marekani CIA, Snowden bado unaendelea.Jee mtu huyo anastahili kupewa hifadhi ya ukimbizi? Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni yao.

Edward Snowden,alietoboa siri za mashirika ya ujasusi ya Marekani
Edward Snowden,alietoboa siri za mashirika ya ujasusi ya MarekaniPicha: Reuters

Gazeti la"Nordwest" linasema aliekuwa mfanyakazi wa shirika la ujasusi la Marekani CIA, Edward Snowden,aliefichua siri juu ya kupelelezwa kwa mawasiliano ya faragha ya simu na kwenye mtandao ametenda usaliti. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba Snowden anatafutwa kwa kutenda uhalifu.Na kwa hivyo serikali ya Ujerumani ipo sahihi, kukataa kumpa Snowden hifadhi ya ukimbizi. Mhariri wa gazeti hilo anasema Snowden siyo shujaa.

Lakini mhariri wa gazeti la "Frankfurter Rundschau" anasema Snowden amewaonyesha mamilioni ya watu kwamba maisha yao ya faragha, kwa kweli siyo ya faragha mbele ya idara ya Marekani ya usalama wa taifa.Na kwa hivyo yeye siyo msaliti,bali anastahiki kusaidiwa.

Viongozi watakiwa kuonyesha msimamo:

Naye mhariri wa "Der Tagesspiegel" anawataka viongozi wa nchi za Ulaya waonyeshe msimamo.Mhariri huyo anaeleza kuwa viongozi wa Ulaya hawapaswi kukiri tu na kusema kuwa walijua kwamba upelelezi ulikuwa unafanywa na mashirika ya Marekani katika nchi zao, ati kwa sababu idara za ujasusi za nchi za Ulaya pia zinayafanya hayo hayo! Viongozi wa Ulaya wanapaswa kumwondolea, Edward Snowden,adha inayomsibu kutokana na jinsi anavyotendewa na Rais Putin nchini Urusi. Siku nyingi mtu huyo alipaswa kupewa anachostahili: yaani hifadhi ya kisiasa.

Juu ya Snowden gazeti la "Cellesche" linatilia maanani kwamba alichokifichua kimewakasirisha watu wengi, lakini, la kusikitisha ni kwamba inapohusu kumsaidia, kwa kumpa hifadhi ya ukimbizi ,wale waliokasirishwa, wanafyata mikia na kukunjika mbele ya Marekani.

Ukosefu wa ajira:

Mkutano wa kulijadili suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wa barani Ulaya ulifanyika jana(Jumanne) mjini Berlin. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linasema kwa waandamanaji katika miji ya Athens, Rome na Madrid, Kansela wa Ujerumani Angela Marekel alionekana kama zimwi. Na kwa hivyo mkutano huo wa mjini Berlin utachangia katika kuyaondoa mawazo kama hayo. Ni wazi kwamba Merkel hatalifungua pochi haraka. Lakini yeye na Waziri wake wa ajira wameahidi msaada

.Na mhariri wa gazeti la "Die Welt" anasema ni jambo zuri kwamba mkutano wa kulijadili tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana umefanyika nchini Ujerumani-nchi inayoshutumiwa na nchi nyingine za Ulaya kwa kuitetea sera ya kubana matumizi Mkutano huo umeonyesha kwamba Ujerumani siyo nchi yenye Kansela mwenye roho ya chuma. Umeonyesha kwamba anayajali matatizo ya vijana wa barani Ulaya.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW