1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Ujerumani kushinda Kombe la Dunia

Abdu Said Mtullya15 Julai 2014

Wahariri leo wanatoa maoni yao juu ya ushindi wa Ujerumani katika mashindano ya kuligombea Kombe la Dunia na juu ya mdahalo wa mabadiliko ya tabia nchi

Mashabiki wa kandanda wawalaki wachezaji wa timu ya Ujerumani mjini Berlin
Mashabiki wa kandanda wawalaki wachezaji wa timu ya Ujerumani mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Rheinpfalz" linasema kandanda siku zote ni ishara yenye nguvu. Na kwa hivyo ushindi wa kombe la dunia katika mwaka huu wa 2014 ni mfano hai wa uthabiti wa Ujerumani kama ambavyo ilivyo imara kwa sasa kisiasa na kiuchumi. Ujerumani ina hadhi kubwa barani Ulaya na duniani kote.Mageuzi yaliyofanyika katika kandanda nchini Ujerumani ni sawa na mageuzi yaliyofanyika katika jamii nzima.

Mhariri wa "Berliner Morgenpost" pia anatilia maanani kwamba ushindi wa timu ya Ujerumani utachangia katika kuleta hisia nzuri katika jamii.

Mhariri huyo anaeleza kwamba ushindi wa kwanza wa timu ya Ujerumani katika mashindano ya Kombe la Dunia mnamo mwaka wa1954 ulikuwa kielelezo cha hisia za kuzaliwa nchi mpya baada ya kumalizika vita kuu vya pili.

Ushindi wa mwaka wa 1974 ulikuwa wa zama za muujiza wa kiuchumi na Ujerumani ilipolibeba Kombe la Dunia mnamo mwaka wa 1990 Wajerumani ndiyo walikuwa wanaungana tena. Na ushindi wa safari hii, japo hauna nahau ya kihistoria, unachangia katika hisia nzuri katika jamii.Na mbali na uhodari uwanjani wachezaji wa Ujerumani wameonyesha tabia nzuri- iliyosimama mbali sana na majikwezo.

Timu yawapa moyo wote

Mhariri wa "Donaukurier anasema kila shabiki wa kandanda analikumbuka vizuri zaidi, tukio fulani la mashindano ya nchini Brazil. Lakini mhariri huyo anahoji kuwa , wote wanakubaliana juu ya jambo moja kwamba jinsi timu ya Ujerumani ilivyocheza imewatia moyo wote. Kila mmoja aliuweka kando ubinafsi, kwa manufaa ya jumuiya.

Mabadiliko ya tabia nchi

Juu ya suala la mabadiliko ya tabia nchi katika muktadha wa mhadalo juu ya mambo ya hali ya hewa unaofanyika mjini Berli mhariri wa "Braunschweiger" anasema licha ya mageuzi ya nishati yaliyofanyika nchini Ujerumani,hatua ya kuridhisha bado haijafikiwa. Mhariri huyo anasema gesi inayoharibu mazingira imeongezeka.

Anaeleza kuwa Ujerumani haitayafikia malengo yake juu ya mabadiliko ya tabia nchi hadi mwaka wa 2020. Sababu ni kwamba kwa viwanda vya wauzaji wa nishati, njia za zamani ndizo zinazoleta faida,yaani kuzalisha nishati kwa kutumia makaa ya mawe .Na ili kuibadilisha hali hiyo,panahitajika mageuzi ya haraka kwenye Umoja wa Ulaya. Lakini ,mahiri huyo anahoji, kwa kuwa Ujerumani ilisuasua juu ya hilo Umoja wa Ulaya nao unasema hauna haraka.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW