Ugiriki yadai fidia
12 Machi 2015Mafashisti wa Ujerumani waliikalia Ugiriki wakati wa vita kuu vya pili. Walisababisha madhara makubwa katika miundo mbinu ya nchi hiyo, walitenda uhalifu wa kivita na pia waliilazimisha Ugiriki kuipa Ujerumani mkopo. Sasa Ugiriki inadai fidia.
Juu ya madai ya Ugiriki gazeti la "Rhein Necker" linasema serikali ya nchi hiyo inafanya kila kitu ili kupata fedha. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba serikali ya Ugiriki imetishia kuzitwaa mali za Ujerumani nchini Ugiriki ikiwa haitalipwa fidia. Mhariri huyo anaishauri Ugiriki iendelee na sera ya mageuzi ili iweze kuyatatua matatizo yake.
Juu ya madai ya fidia yanayotolewa na Ugiriki kwa Ujerumani, mhariri wa gazeti la "Westfalenpost" anauliza iwapo Ugiriki inafanya hivyo kutokana na kutamauka? Na anasema kwamba nchi za Ukanda wa sarafu ya Euro hazipo tayari kutoa fedha zaidi kwa ajili ya Ugiriki.
Wenye madeni wawe na nadhari
Naye mhariri wa gazeti la "Thüringischen Landeszeitung" anazitaka nchi zinazokabiliwa na migogoro ya madeni ziwe na nadhari.Mhariri huyo anaeleza kwamba nchi zinazokabiliwa na matatizo ya fedha zinapaswa kuwa na uangalifu ili ziepushe kuuharibu kabisa uhusiano baina yao na Ujerumani na nchi nyingine za Ukanda wa sarafu ya Euro. Ugiriki inapaswa izungumzie juu ya msaada inaoweza kuupata kutoka Umoja wa Ulaya badala ya kuliingiza suala la fidia katika mazungumzo hayo.
Ujerumani pia ilisamehewa madeni baada ya vita
Mhariri wa gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" anasema suala la fidia baina ya Ugiriki na Ujerumani lilitatuliwa miaka mingi iliyopita. Lakini mhariri wa gazeti la "Nürnberger Nachrichten" anasema ngoja kwanza! Na anakumbusha kwamba bila ya kusamehewa madeni yake ,baada ya vita Kuu vya pili,Ujerumani isingeliweza kuinuka tena. Na kwa hivyo bila ya Ugiriki kusamehewa madeni yake nchi hiyo haitapata uzima tena. Kwa kudai fidia,Ugiriki inakumbusha kwamba Ujerumani pia ilisamahewa madeni yake.
Maadhimisho ya "Siku ya ushindi dhidi ya Hitler "
Jee ni sahihi kwa Kansela wa Ujerumani kukataa kushiriki katika maadhimisho ya siku ya ushindi dhidi ya Hitler? Gwaride la maadhimisho hayo litafanyika mjini Moscow tarehe tisa ya mwezi Mei. Mhariri wa gazeti la "Sächsiche" anasema Kansela Merkel amefanya uamuzi sahihi kutohudhiria gwaride hilo ili kujieweka kando na serikali ya Urusi.
Mhariri anasema lakini pia ni uamuzi sahihi kwa Kansela Merkel kwenda kwenye makaburi ya askari wasiojulikana na kuweka mashada ya maua ili kuonyesha heshima. Isingelikuwa sahihi kwa Angela Merkel kuketi kwenye jukwaa karibu na Rais Putin na kuziangalia silaha zile zile za Putin zinazouhujumu uhuru wa Ukraine.
Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Yusuf Saumu