Magazetini.
29 Juni 2009Vyama vya kihafidhina vilivyomo katika serikali ya Ujerumani vimetangaza programu ya uchaguzi mkuu utakaofanyika hapa nchini Ujerumani mnamo mwezi septemba . Wahariri wa magazeti ya hapa nchini wanazungumzia suala hilo katika maoni yao leo.
Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya utayarifu wa Marekani katika kufanikisha juhudi za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU vilivyomo katika serikali ya mseto hapa nchini vimeahidi kupunguza kodi ya mapato, kama sehemu ya kampeni ya uchaguzi mkuu.
Juu ya kampeni hiyo gazeti la Emder linasema vyama vya CDU na CSU vimekubaliana juu ya kupunguza kodi lakini gazeti linasema vyama hivyo havikutaja tarehe ya kuanza kutekeleza ahadi hiyo.
Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa ikiwa, vyama hivyo havitaji tarehe maalumu juu ya kutekeleza ahadi yao, itakuwa vigumu kwa wapiga kura kusema ahadi hiyo ni hadaa za kampeni za uchagazi. Baada ya uchaguzi vyama hivyo vitakuwa na muda wa kufikiria juu ya ahadi yao.
Mhariri wa gazeti la Emder anasema iwapo wapiga kura watakubali hayo itaonekana baada ya uchaguzi.
Hatahivyo mhariri wa gazeti la Sächsische anasema, ikiwa mtu alifuatilia kwa makini hotuba ya mwenyekiti wa chama cha CDU Angela Merkel ameweza kutambua kwamba mwenyekiti huyo hakusema chochote.
Gazeti hilo linaeleza kuwa hakuna mtu anaejua kwa uhakika ni lini Ujerumani itaondokana na mgogoro wa uchumi.Kwa hiyo ahadi juu ya kupunguza kodi haikufafanuliwa, vipi na lini itatekelezwa.
Gazeti la Münchner Merkur linasema katika mazingira magumu ya mgogoro wa uchumi ni vigumu kuona ni lini na vipi ahadi ya kupunguza kodi inaweza kutimizwa. Mhariri wa gazeti hilo anawaonya wanasiasa kuwa wasishangae ikiwa wananchi watawakasirikia kwa kujaribu kufikiri kwamba wao ni wapumbavu.!
Katika maoni yake mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker anazungumzia juu ya ishara ya matumani kutoka Marekani kabla ya kufanyika mkutano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa .
Mhariri huyo anasema pana ishara ya matumaini kutoka Marekani juu ya mkutano utakaojadili mabadiliko ya hali ya hewa mjini Copenhagen.
Gazeti la Neue Osnabrücker linaeleza kuwa rais Obama anatambua kwamba nishati endelevu ziteleta nafasi za kazi. Marekani imo mbioni kuwa wa kwanza katika tekinolojia ya nishati ya upepo.Gazeti linasema hayo ni matumaini makubwa kutoka Marekani katika kufanikisha mkutano juu ya mabadiliko ya hali hewa utakaofanyika mjini Copenhagen mwishoni mwa mwaka huu.
Mwandishi:Abdul Mtullya/Dt Agenturen
Mhariri:Abdul-Rahman