Magazetini
13 Januari 2010Miaka 30 iliyopita watu waliokuwa na mitazamo tofuati waliamua kuziweka kando tofauti zao na kuunda jumuiya ya kutetea mazingira- Chama cha kijani. Jee chama hicho kimefanya nini baada ya miaka 30. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni yao.
Gazeti la Allgemeine Zeitung, linakumbuka kwamba watu mbalimbali, ikiwa pamoja na wakomunisti, watetea haki za wanawake, wapenda amani, na wengine walikutana miaka 30 iliyopita ili kuanzisha jumuiya ya kuikoa dunia. Gazeti la Allgemeine Zeitung linakumbuka kwamba hakuna aliefikiri kuwa jumuiya hiyo ingelikuwa na uhai mrefu. Pamoja na hayo watu hao walidhihakiwa, na hata walilaaniwa.
Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema uamuzi wa kuunda jumuiya ya watetea mazingira miaka 30 iliyopita ulikuwa sahihi kwa Ujerumani.Mhariri huyo anasema siyo lazima mtu akubaliane na kila sera inayowakilishwa na chama cha kijani. Lakini chama hicho kinayazungumzia masuala ambayo vyama vingine vinayapuuza ,vinayafanyia ajizi au kuyafunika- masuala muhimu kwa mustakabal wa mwanadamu.
Lakini gazeti la Frankfurter Neue Presse linauliza, jee bado tunakihitaji chama cha kijani?
Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba swali hilo limekuwa linaulizwa tokea malengo ya chama cha kijani yalipoanza kuungwa mkono , siyo tu na watu katika chama cha Social Democratic SPD, bali pia na watu katika vyama vya CDU na CSU. Jibu la swali hilo: ni "NDIYO," wanamazingira bado wanahitajiwa. Sababu ni kwamba bila ya chama chao kuwapo, vyama vingine vitadeka.
Hatahivyo mhariri wa Franfurter Neue Presse anasema pamoja na hayo yote, wanamazingira wanahitaji jambo moja muhimu : wanahitaji uongozi mpya.
Mhariri anaeleza kuwa chama cha kijani kinaadhimisha mwaka wa 30 tokea kuundwa kwake nchini Ujerumani, lakini waasisi wake wamefikia wastani wa umri wa miaka 60
Gazeti linaeleza kuwa kwa muda mrefu vijana waliwekwa kando. Gazeti linasema ikiwa nguvu za vijana hazitaingizwa katika chama, basi chama hicho kitawachusha watu.
Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri/: Othman, Miraji