Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.
28 Januari 2010Mkutano wa kimataifa juu ya Afghanistan unafanyika mjini London leo , pamoja na masuala mengine, kujadili njia za kuwakaribia wataliban.
Wahariri wa magazeti ya hapa nchini wanatoa maoni yao juu ya mkutano huo.
Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya hotuba iliyotolewa jana na rais Shimon Peres wa Israel kwenye bunge la Ujerumani katika maadhimisho ya mwaka wa 65 tokea kukombolewa kwa watu waliokuwa wamefungwa katika kambi ya Auschwitz nchini Poland.
Juu ya mkutano unaojadili suala la Afghanistan mjini London gazeti la Rhein-Necker linasema , kuwa mkutano huo hautaisogeza Afghanistan kwenye hatua ya amani, badala yake mkutano huo unatumiwa na nchi za magharibi kwa maslahi yao ya kisiasa.Gazeti hilo linaeleza kuwa mkutano huo ni jukwaa la kisiasa linalotumiwa na nchi za magharibi kwa lengo la kufafanua mkakati wa kujiondoa Afghanistan.
Gazeti la Süddeutsche Zeitung linatilia maanani kwamba rais Karzai anajaribu kutafuta njia ya kuwakaribia wataliban. Gazeti linasisitiza kwamba hilo ni jukumu la rais huyo kwa sababu haiwezekani kwake kuendelea kwa muda mrefu zaidi kutegemea kulindwa na majeshi ya nchi za nje. Gazeti hilo linaeleza kwamba kinachowezekana kufanyika nchini Afghanistan ni kujaribu kuwaingiza wataliban katika jamii na kujaribu kuwatengenaisha na alkaida; lakini zaidi ya hayo hakuna kinachoweza kufanyika nchini humo.
Gazeti la Märkische Oderzeitung linazungumzia juu ya mkutano uliofanyika jana , pia mjini London, kuhusu Yemen. Gazeti hilo linasema Yemen imegeuka kuwa nchi isiyokuwa na matumaini kama Somalia kwa sababu kwa muda mrefu, hakuna alietaka kujua kilichokuwa kinaendelea katika nchi hiyo. Lakini sasa wakati dunia inataka kujua kinachotokea, mambo yameshaenda mrama.
Umasikini unaongezeka kutokana na kupungua kwa mapato yanayotokana na mauzo ya mafuta. Mhariri wa gazeti la Märkische Oderzeitung anasema umasikini ndio unaowafanya watu zaidi na zaidi wajiunge na makundi ya wanaitikadi kali wa kiislamu. Gazeti linasema, ndiyo serikali ipo nchini humo, lakini inazidi kupoteza udhibiti wa nchi.
Rais Shimon Peres wa Israel jana alilihutubia bunge la Ujerumani katika maadhimisho ya mwaka wa 65 tokea kukombolewa kwa kambi ya Auschwitz iliyotumika kuwaangamiza maalfu kwa maalfu ya watu na hasa wayahudi. Katika hotuba yake rais huyo alitoa mwito wa kuendelea kuwakumbuka wahanga wa Auschwitz. Gazeti la Kieler Nachrichten linaeleza kuwa sababu ya kutoa mwito huo ni kwamba wapo watu nchini Ujerumani wanaofikiri kwamba kumbukumbu juu ya maangamizi ya wayahudi siyo jambo la lazima sana. Lakini mhariri wa gazeti la Aachener anasema asietaka kuyakumbuka maangamizi ya wayahudi hasikii vizuri.
Mhariri wa gazeti hilo anasisitiza umuhimu wa hotuba ya rais Peres pia kutokana na kutambua ukweli kwamba wapo watu nchini Ujerumani wanaojaribu kufananisha unyama waliofanyiwa wayahudi na masaibu ya wapalestina.
Mwandishi/Mtullya Abdu /Deutsche Zeitungen.
Mhariri/Othman Miraji