1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Karadzic/CeBIT

Abdu Said Mtullya2 Machi 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya maonyesho makubwa ya tekinolojia CeBIT.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwenye maonyesho ya tekinolojia mjini Hannover.Picha: AP

Wahariri magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya kesi inayomkabili aliekuwa kiongozi wa Serbia, Karadzic, na juu ya maonyesho makubwa ya tekinolojia CeBit yanayoendelea katika mji wa Hannover.

Aliekuwa kiongozi wa Bosnia -Serbia, Radovan Karadzic,jana alianza kujitetea mbele ya mahakama ya kimataifa ya mjini the Hague jana.

Karadzic anakabiliwa na tuhuma za mauaji halaiki ya maalfu ya Waislamu, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mashtaka mengine kadhaa.

Karadzic aliiambia mahakama kwamba vita vya Bosnia vilikuwa halali na vitakatifu!

Juu ya kauli hiyo, mhariri wa gazeti la Westfälische Nachrichten anasema Karadzic anajaribu kuzitupia lawama nchi za magharibi kwa mauaji yaliyotokea.

Sababu ya kufanya hivyo ni kutafuta kuungwa mkono na watu wake, yaani Waserbia. Gazeti linasema , hiyo hasa ndiyo sababu anashikilia kwamba anayoyasema katika kujitetea yatafsiriwe ili ujumbe ufike nyumbani yaani kwa watu wake.

Lakini gazeti la Westfälische Nachirichten linasema udhalimu unaowakilishwa na Karadzic kama ushujaa ni kipingamizi katika juhudi za kuingia katika Ulaya huru na ya kidemokrasia.

Hata hivyo, gazeti la Saarbrücker linatoa tahadhari kwa mahakama ya kimataifa kwa kueleza kuwa Karadzic anadai kwamba nchi za Nato zilibuni unyama uliotendeka ili kupata sababu ya kuishambulia nchi yake.Gazeti hilo linasema mahakama ya kimataifa,ICC, inapaswa kuwa macho juu ya madai kama hayo, kwa sababu ikiwa Karadzic atafanikiwa kulidhibiti jukwaa, mahakama hiyo inaweza kupoteza uadilifu wake.

Gazeti la Badische Neueste Nachrichten linatoa maoni juu ya maonyesho makubwa ya Kompyuta CeBIT, yanayofanyika kila mwaka katika mji wa Ujerumani, Hannover. Lakini gazeti hilo linayazungumzia maonyesho hayo kuhusiana na mjadala juu ya kulinda data za wananchi.

Gazeti hilo linasema tekinolojia inaweza kuwa nzuri au mbaya. Hayo yanategemea na mtumiaji. Hatahivyo inapasa kusisitiza kwamba huduma ya mtandao wa internet sasa imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku na inatoa mchango mkubwa katika kutatua migogoro ya zama zetu.

Na mhariri wa gazeti la Leipziger Volkszeitung anasema ni jambo la busara kwamba viongozi wa Ujerumani wanalitilia maanani suala la data za wananchi.

Mhariri huyo anaeleza kuwa tume inayohusika itapaswa ifafanue jinsi jamii ilivyobadilika kutokana na matumizi ya mtandao wa internet.

Na gazeti la Rhein Necker linazingatia hoja ya kiuchumi kuhusu maonyesho ya kompyuta- CeBIT .Na linasema kuwa licha ya kupungua kwa washabiki na waonyeshaji, maonyesho ya kompyuta CeBIT bado ni muhimu kwa uchumi wa Ujerumani.

Kwani katika miaka mitano ijayo nafasi za ajira zipatazo laki moja zitatokana na sekta hiyo.

Mwandishi/Mtullya Abdu /DZ

Mhariri: Miraji Othman


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW