1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Abdu Said Mtullya20 Aprili 2010

Jee jambo gani ni muhimu, fedha au uhai wa mwanadamu?Wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao juu ya swali hilo.

Abiria waliokwama kwenye uwanja wa ndege wa Kiev-BorispolPicha: DW

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya athari zinazotokana na hatua ya kupiga marufuku safari za ndege.Mashirika ya ndege sasa yanalalamika juu ya hasara yanayoyapata kufuatia hatua ya kupiga marufuku safari za ndege.

Gazeti la Schwäbische Zeitung linasema madhali wataalamu bado hawajakuwa na uhakika, juu ya wakati gani wingu la jivu litaondoka,jambo la kufanya sasa ni moja tu ; nalo ni kuzingatia usalama. Kwa hiyo mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba vitisho vinavyotolewa na mashirika ya ndege ni jambo la kijuvi.

Mashirika hayo yanataka safari za ndege zianze tena, lakini mhariri wa gazeti la Schwäbische anasema ni kweli kwamba hasara ya mamilioni ya fedha ni jambo linalotia uchungu,lakini hasara kubwa zaidi ni kupotea kwa maisha ya binadamu.

Mhariri wa gazeti la Flensburger Tageblatt anauliza "jee kitu gani ni muhimu,fedha au usalama"?Na anasema jibu la swali hilo ni moja tu !

Mhariri huyo anasema madhali hakuna uhakika juu ya usalama,ni sawa kuendelea kupiga marufuku safari za ndege hata ikiwa mashirika ya ndege yanaingia hasara kubwa.Lakini mhariri huyo anasema Ujerumani inaweza kuhimili hasara hiyo kwa siku hizi chache,kwani volkano haitaripuka tena,mvua itanyesha na italiondoa jivu ;anga itakuwa salama na ndege zitapaa na zitatua salama.

Katika maoni yake mhariri wa gazeti la Wiesbadaner Kurier anazungumzia juu ya safari za majaribio zilizofanywa na baadhi ya mashirika ili kuona iwapo inawezekana kuzianzisha tena safari za ndege.

Mhariri huyo anasema hata safari hizo za majaribio zinapaswa kupigwa marufuku inapohusu usalama wa watu.

Gazeti hilo linakumbusha juu ya mikasa ya miaka mingi ya nyuma, ambapo ndege kubwa za abiria zilikaribia kuanguka kutokana na jivu la volkano.

Jee serikali inawajibika kuyasaidia mashirika ya ndege kukabiliana na hasara iliyotokana na hatua ya kupiga marufuku safari za ndege? Mhariri wa gazeti la Financial Times Deutschland anauliza swali hilo?

Mhariri huyo anakiri kwamba kulinganisha na mgogoro wa mabenki,mzigo wa kuyasaidia mashirika ya ndege ungelikuwa mdogo japo mhariri anakumbusha kuwa mgogoro huo umesababishwa na janga la asili.Na hiyo ati ndiyo iwe sababu kwa serikali kuyasaidia mashirika ya ndege. Hapana anasema mhariri huyo,huko kutakuwa kwenda mbali mno!

Serikali inapaswa ,kusaidia ikiwa uchumi wote wa nchi umo katika hatari ya kuathirika.

Mhariri wa Financial Times Deutschland anasema asilani, mlipa kodi asibebeshwe zigo la kudumisha uhai wa mashirika ya ndege yanaoingia hasara!

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri/Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW