Maoni ya wahariri
5 Septemba 2013Gazeti la "Der Tagesspiegel" linazungumzia juu ya ziara ya Rais wa Ujerumani Joachim Gauck nchini Ufaransa. Rais huyo ameitembelea sehemu ya magofu ya kijiji cha Oradour sur- Glane ambako mafashisti wa Ujerumani walifanya mauaji halaiki mnamo mwaka wa 1944. Katika maoni yake mhariri wa gazeti la "Der Tagesspiegel"anatilia maanani kwamba Joachim Gauck ndiyo Rais wa kwanza wa Ujerumani kuitembelea sehemu hiyo ya fedheha. Mhariri huyo anasema serikali za Ujerumani bado zinaendelea kukataa kuwalipa fidia waliofikwa na maafa ya uvamizi wa mafashisti kwa kutoa sababu zisizokuwa na uzito. Anasema ni kweli kwamba Rais Gauck hawezi kuibadilisha hali hiyo,lakini angalau anaweza kutoa ishara ya nia njema kwa kufanya ziara katika sehemu hiyo ya aibu.
Wakimbizi wa Syria
Gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger" linatoa maoni juu ya mwito uliotolewa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya ziufuate mfano wa Ujerumani katika kuwasaidia wakimbizi wa Syria. Ujerumani ipo tayari kuwapokea wakimbizi alfu tano wa Syria.
Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba hatua ya Kansela Merkel ya kujisifu mwenyewe siyo sahihi.Kwani inapasa kuilinganisha idadi hiyo ya wakimbizi alfu tano na ukubwa wa tatizo la wakimbizi nchini Syria kwa jumla.Kujisifu kwa Kansela Merkel pia siyo sahihi kwani kwa muda mrefu serikali ya Ujerumani haikutaka kuwa na habari zozote juu ya wakimbizi wa Syria, na badala yake ilipendelea wakimbizi hao wapelekwe katika nchi nyingine za Umoja wa Ulaya. Na hata kwenye Umoja wa Ulaya, Ujerumani haikuchukua hatua ili kutafuta mkakati wa kijasiri wa pamoja, juu ya kulishughulikia suala la wakimbizi wa Syria.
Jaribio la kombora la Israel
Israel ilirusha kombora kutokea bahari ya Mediterania wakati wa mazoezi ya pamoja na jeshi la Marekani. Lengo la jaribio hilo ni kuupima ulinzi dhidi ya makombora. Lakini mhariri wa gazeti la "Nürnberger Nachrichten" ana maoni tofauti, na anasemkuwa anaefikiria kwamba kufanya mashambulio ndiyo njia ya kuichagua, basi hana budi awe tayari pia kuyafikiria matokeo yake.Jee kuna mtu anaefikria kwamba mazungumzo ya kuleta amani yaliyoanza hivi karibuni baina ya Israel na Wapalestina yataendelea? Swali hilo linahusu pia mazungumzo ya kuutatua mgogoro unaotokana na mpango wa nyuklia wa Iran. Jaribio la kombora la Israel linaweza kusababisha madhara ya muda mrefu sana.
Ubadhirifu wa fedha Uhispania
Na mhariri wa "Münchner Merkur" anauliza katika maoni yake,kulikoni,Uhispania?Watu milioni sita hawana kazi nchini humo, watu wa Ulaya walitoa Euro Bilioni 40 ili kuyaokoa mabenki ya Uhispania .Ligi ya Uhispania inadaiwa Euro milioni 700.Na sasa inakuaje timu moja tu-yaani Real Madrid inamnunua mchezaji kwa Euro Milioni 91? Mhariri wa gazeti la "Munchner Merkur" anasema ni sawa kabisa kwa watu, barani Ulaya kukasirika!
Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Josephat Charo