1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya15 Oktoba 2013

Wahariri leo wanazungumzia juu ya juhudi za kuunda serikali ya mseto nchini Ujerumani,mkutano baina ya Iran na nchi za magharibi na juu ya chama cha mrengo mkali wa kulia nchini Ufaransa

Wajumbe wa vyama vya kihafidhina na wa chama cha Kijani
Wajumbe wa vyama vya kihafidhina na wa chama cha KijaniPicha: Reuters

Gazeti la "Rhein-Necker linatoa maoni juu ya mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto nchini Ujerumani. Hapo jana wajumbe wa vyama vya kihafidhina walikutana na wajumbe wa chama kikuu cha upinzani cha SPD. Na leo wajumbe wa vyama vya kihafidhina wanakutana na wawakilishi chama cha watetezzi wa mazingira, cha kijani

Mhariri wa gazeti la "Rhein-Necker" analitilia maanani suala la mishahara ya kima chini kama jinsi linavyowasilishwa na wajumbe wa chama cha SPD kwenye mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto. Mhariri huyo anasema msimamo wa chama cha SPD wa kuling'ang'ania suala hilo unaonyesha dhamira ya chama hicho ya kutaka kuzishika hatamu za serikali pamoja na vyama vya CDU na CSU.

Mhariri wa gazeti la "Saarbrücker" anazungumzia uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya mseto baina ya chama cha Kansela Angela Merkel,CDU,chama ndugu cha CSU na chama cha watetezi wa mazingira. Lakini mhariri huyo anakitahadharisha chama cha kijani kwa kueleza kwamba chama cha kijani sasa kimekuwa sehemu thabiti ya siasa za msingi nchini Ujerumani.Lakini kuingia katika mradi wa serikali ya mseto na vyama vya kihafidhina ni mapema mno kwa chama hicho na wala hakijajiandaa vizuri.Mradi huo utakigawanya chama hicho na kusababisha kiupoteze wajihi wake asilia.

Mgogoro wa nyuklia

Gazeti la "Nordwest"linatoa maoni juu ya mazungumzo ya mgogoro unaotokana na mpango wa nyukilia wa Iran.Mhariri wa gazeti hilo anasema hatua ya kufanyika tena kwa mazungumzo hayo ni mafanikio ya juhudi za nchi za magharibi.Vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na nchi hizo dhidi ya Iran vimesababisha madhara katika uchumi wa Iran ,badala ya kuwaimarisha wale wenye itikadi kali katika uongozi wa Iran, kama baadhi ya watu wanavyoamini. Wenye siasa za wastani sasa wanaweza kujaribu kuyatekeleza malengo yao. Hata hivyo nchi za magharibi zinapaswa kuendelea na shinikizo. Na mhariri wa "General-Anzeiger" anaongeza kwa kusema kwamba litakuwa kosa kwa nchi za magharibi kuzilegeza sukurubu za vikwazo dhidi ya Iran.

"National Front" Ufaransa

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatoa maoni juu ya ushindi wa chama cha mrengo mkali wa kulia, cha "National Front" katika uchaguzi mdogo nchini Ufaransa.Gazeti hilo linapiga mbiu ya mgambo katika maoni yake

Linasema mwaka ujao uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika nchini Ufaransa. Hatari kwa chama cha Wasoshalisti ni kubwa kutokana na udhaifu katika kazi iliyofanywa na serikali yao.Wafaransa wengi wamevunjika moyo kutokana na ukosefu wa ajira,kupandishwa kodi na kushindwa kwa serikali ya Wasoshalisti kuyatekeleza mageuzi. Wasoshalisti wamo hatarini kuadhirika katika uchaguzi wa bunge la Ulaya.Chama cha mrengo mkali wa kulia cha "National Front" sasa kinatishia kuchukua nafasi za mbele katika siasa za Ufaransa.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen .

Mhariri: Abdul-Rahman :

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW