Maoni ya wahariri
16 Januari 2014Bunge la Ulaya limeidhinisha mpango wa kupunguza kwa asilimia 28 hewa chafu inayosababishwa na magari makubwa kuanzia mwaka wa 2020.
Kulingana na utaratibu unaokusudiwa magari yote yenye ukubwa wa kati yanayouzwa barani Ulaya yatatoa kiasi ya gramu147 za hewa chafu badala ya gramu 203 kuanzia mwaka wa 2007.
Juu ya utaribu huo mhariri wa gazeti la "Neue Ruhr" anasema Ulaya inatoa ishara duniani kuonyesha kwamba ulinzi wa mazingira siyo muhimu sana.Ishara hiyo itawazuia wawekaji vitega uchumi wanaohitaji uhakika katika mipango yao inayohusu nishati za jua,upepo na maji kwa ajili ya mitambo yao.
Mhariri huyo anasema mpango wa Umoja wa Ulaya utachochea ujenzi wa vinu vya nyuklia kwa sababu nchi kama Ufaransa na Uingereza hazina imani na tekinolojia za mashaka zinazopendekezwa kwa ajili ya kupunguza hewa chafu.
Gazeti la "Westdeutsche" linasema mpango wa Umoja wa Ulaya utaleta manufaa kwa wenye viwanda tu na mwananchi wa kawaida atatoka patupu. Mhariri wa gazeti hilo anasema mpango wa Umoja wa Ulaya utauzuia mchakato wa kuleta mageuzi katika sekta ya nishati na hatimaye mpango huo utakuwa wa mashaka makubwa.
Naye mhariri wa gazeti la "Südwest Presse" anaungalia mpango wa kulinda mazingira wa Umoja wa Ulaya kwa jicho la Ujerumani. Anaeleza kwamba mpango huo asilani haulingani na malengo ya Ujerumani.Awali ya yote inapasa kutilia maanani kwamba mageuzi ya nishati nchini Ujerumani yanalenga shabaha ya kutenga nafasi za ajira na kuzidumisha zilizopo.
Ubakaji India
Na sasa tugeukie India ambako kwa mara nyingine mwanamke amebakwa na genge la wanaume. Mama huyo alikuwa mtalii kutoka Denmark.
Juu ya mkasa huo mhariri wa gazeti la "Dresdner Neueste Nachrichten" anasema kadhia hiyo inaonyesha jinsi wanawake wanavyoshushwa thamani nchini India. Mhariri huyo anahoji kuwa ubakaji wa wanawake siyo jambo linalotokea katika nchi zinazoendelea tu. Lakini vitendo vya mara kwa mara, vya magenge ya wanaume kumkalia mwanamke mmoja kipopo, hasa nchini India ni ishara ya kumshusha thamani mwanamke.
Matumaini nchini Ujerumani
Gazeti la "Nordwest " linazungumzia juu ya uchumi wa Ujerumani. Mhariri wa gazeti hilo anasema ustawi wa asilimia 0.4 mwaka uliopita umeleta matumaini yenye msingi thabiti: watu wengi wana ajira, Ujerumani imeendelea kuwa nguzo imara ya kiuchumi barani Ulaya na imeweza kuuza biadhaa nje kwa kiwango kikubwa. Kinachohitajika sasa ni kuuimarisha msingi huo.
Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen:
Mhariri:Yusuf Saumu