Maoni ya wahariri
2 Desemba 2014Gazeti la "Nürnberger Nachrichten"linatoa maoni juu ya uamuzi wa Mahakama ya kimataifa ya mjini the Hague wa kuikataa rufani ya aliekuwa mbabe wa kivita Thomas Lubanga aliewatumia watoto kama askari katika jeshi lake la uasi.Ndiyo kusema Lubanga ataendelea kukitumukia kifungo jela.
Ukosefu wa miundo mbinu katika sekta ya sheria
Mhariri wa "Nurnberger Nachrichten" anasema kesi ya Lubanga kwenye Mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague imeoinyesha mipaka ya mahakama , na wakati huo huo imetoa onyo kwa waendesha mashata. Kwani licha ya matatizo na ugumu uliopo waendesha mashtaka wanapaswa kutumia njia za ufanisi zaidi za kuwasilisha ushahidi ili kuzithibitisha tuhuma zao.
Mhariri huyo anasema haitoshi kuwapeleka waendesha mashatka kwenye nchi iliyomo katika vurumai za kisheria na kijamii ,ambamo hakuna majalada juu ya uhalifu na wala hakuna mashahidi wa kuaminika.
Edward Snowden
Gazeti la " Donaukurier" linazungumzia juu ya hati za siri zilizofichuliwa na aliekuwa wakala wa shirika la ujasusi la Marekani . Mhariri wa gazeti hilo anasema shughuli za upelelezi za kiwango kikubwa za mashirika ya ujasusi ya Marekani, Uingereza na kwa kiasi fulani za shirika la ujasusi la Ujerumani zinaonyesha jinsi mambo yalivyoenda mrama.
Mhariri huyo anaeleza kuwa mashirika hayo yamejijengea himaya na hayadhibitiki, kiasi kwamba shughuli zao zinavuka mipaka ya harakati za kupambana na ugaidi.Na kutokana na tekinolojia za kisasa ,sasa inawezekana kwa mashirika hayo kuwachunguza wanacnhi wote kwa ukamilifu katika nchi zao, jambo ambalo lilishindikana kwa shirika la ujasusi la Ujerumani Mashariki "Stasi."
Mabadiliko ya tabia nchi yajadiliwa Lima
Mkutano wa dunia juu ya mabadiliko ya tabia nchi unafanyika mjini Lima nchini Peru. Mhariri wa gazeti la "Die Welt" anasema mkutano huo unapasa kuipa Ujerumani changamoto ili serikali ya nchi hiyo ipitishe sheria haraka sana ,kwa ajili ya kuifunga migodi ya makaa ya mawe na kuvifunga vinu vyote vya nishati ya kinyuklia.
Wakimbizi Ujerumani
Na mhariri wa gazeti la "Mannheimer Morgen"anawazungumzia wakimbizi wanaokuja Ujerumani. Mhariri huyo anatilia maanani kwamba wakimbizi hao wanaliimarisha soko la ajira nchini Ujerumani. Mhariri huyo anasema kuwa Ujerumani ni sumaku inayowavutia wahamiaji kutoka nje, na hasa raia wa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya. Kutokana na sekta za viwango vya chini vya mishahara ni rahisi kwa wahamiaji kupata ajira haraka,zisizohitaji ujuzi wa juu.
Hatahivyo wale wenye ujuzi wa juu wanakabiliwa na matatizo katika kupata kazi. Sababu ni kwamba vyeti vyao havitambuliwi kwa urahisi. Lakini sasa baada ya vyama vya CDU na CSU vilivyomo katika serikali, kuachana na msimamo wao wa upinzani, yumkini wakimbizi wataingizwa katika soko la jira kwa njia nzuri zaidi nchini Ujerumani.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Josephat Charo