Wahariri watoa maoni juu ya uchunguzi wa tuhuma za uhalifu wa kukwepa kodi
27 Februari 2008
Idara za sheria za Ujerumani zinafuatilia kwa uthabiti wote tuhuma za uhalifu wa kukwepa kodi zinazomkabili aliekuwa meneja wa posta Klaus Zumwinkel na watu wengine nchini Ujerumani. Juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda.
Gazeti la KÖLNER STADT-ANZEIGER
linazipongeza idara za sheria kwa kufanya kazi nzuri hadi sasa.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa ushahidi uliopo ni shadidi kama chuma dhidi ya wahalifu . Anatilia maanani kuwa licha ya kiasi cha fedha kilichohusika katika uhalifu huo kuthibitika kuwa ni Euro milioni 200,kazi iliyofanywa na idara za upelelezi imeleta matunda.Hapo awali kiasi kilichotuhumiwa kilikuwa Euro Bilioni nne.
Gazeti linasema utaratibu wa kuweka data kwenye kitengo cha shirika la upelelezi umethibiti kuwa wa mafakinio.
Na mhariri wa gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU anazipongeza idara za sheria Ujerumani kwa kueleza kuwa ingawa hatua iliyofikiwa hadi sasa haionekani kuwa ya kusisimua kulinganisha na ukubwa wa tuhuma za hapo mwanzoni ,idara za sheria za Ujerumani zimeonesha jinsi zinavyofuatilia kwa moyo wote uhalifu wa kukwepa kodi.Katika maoni yake mhariri pia anatilia maanani kuwa maafisa wa idara hizo walianza kwa kufanya msako kwenye nyumba ya mtuhumiwa mkuu, Klaus Zumwinkel aliekuwa meneja wa Posta.
Mhariri anasema juhudi za maafisa hao zimewatikisa mabwana na mabibi fulani hadi Liechtenstein.
Lakini gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE , pamoja na kusifu hatua iliyofikiwa hadi sasa katika uchunguzi, linasikitika kwamba watu waaminifu siku zote ndio wanaopunjika.
Gazeti linasema anaelipa kodi wakati unaotakiwa na kwa kufuata taratibu zilizopo hana anachoambulia kutoka kwa wanakwepa kodi ,badala yake akiba yake ya benki itamulikwa na biashara zake vilevile zitapigwa darubini zaidi na zaidi.
Kwa upande wake Gazeti la STUTTGARTER -ZEITUNG linasema hatua zilizochukuliwa na idara za sheria za Ujerumani katika kufuatilia tuhuma za uhalifu wa kukwepa kodi zitachangia katika kuwafanya wananchi wawe waaminifu na katika maoni yake gazeti la SWARZWÄLDER BOTE linalosema shimo ambamo wahalifu wamekuwa wanaficha fedha sasa limetifuka-shimo hilo ni Liechtenstein.