Magazetini.
7 Mei 2008Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazingatia hasa masuala ya nje.
Lakini wahariri hao pia wanazungumzia juu ya tatizo la watoto wanaokabiliwa na ugumu katika masomo yao nchini Ujerumani.Wengi wanahitaji msaada hata baada ya kumaliza shule.
Gazeti la WESTFÄLISCHER ANZEIGER linazungumzia juu ya Urusi ambapo rais wa hadi sasa Vladimir Putin leo amekabidhi madaraka kwa rais mpya, Dimitry Medvedev.
Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema ,hata kufikiria tu kwamba mabadiliko yanafanyika ni kupiga chuku. Anasema kinachotokea ni kwamba rais huyo mpya anaingia ofisini kuenda kukalia kiti alichosogezewa na Putin. Lakini ukweli ni kuwa Putin ataendelea kushika hatamu za uongozi.
Gazeti hilo linatilia maanani kwamba warusi wanataka mtu kama Putin awe kiongozi wao.
Na kutokana na hayo itakuwa vigumu kwa rais mpya ,Medvedev kuingia madarakani na kutekeleza sera zake.
Gazeti la RHEIN-NECKER ZEITUNG linamzungumzia rais mwengine; Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ambae kwa sasa anaanguka katika umaaruf.
Kura za maoni zinathibitisha hayo. Lakini gazeti hilo linaeleza kuwa, kinachomfanya rais Sarkozy aanguke katika kura za maoni ,siyo hasa siasa zake bali ni mitindo anayotumia katika kutekeleza siasa hizo. Mhariri anasema mara nyingi rais huyo anaonekana kuwa mwingi wa pupa.
Pamoja na hayo kiongozi huyo anaonekana kuwa ametingwa na mambo mengi katika maisha yake ya faragha.
Gazeti la WESTFÄLISCHE NACHRICHTEN linazungumzia juu ya maafa yaliyotokea nchini Mynmar na jinsi utawala wa nchi hiyo unavyokabiliana na maafa hayo.
Mahariri wa gazeti hilo anasema utawala huo umeonesha uzuzu usiosemeka.
Gazeti linasema utawala wa Mynmar ulitumia vyombo vya habari kueneza propaganda juu ya kura ya maoni badala ya kuwaandaa wananchi ili waweze kuyakabili maafa yaliyosababishwa na kimbunga Nargis.
Mhariri anasema wakati watawala hao walipokuwa wanaeendesha propaganda ya kuimarisha utawala wao, kimbunga Nargis kimeendelea kuleta maangamizi.
Gazeti la WESTDEUTSCHE linaeleza wasiwasi juu ya mfumo wa elimu nchini Ujerumani. Linatilia maanani kuwa theluthi moja ya watoto wa shule wanahitaji msaada wa masomo ya ziada. Juu ya hayo gazeti la WESTDEUTSCHE linasema
katika jitihada za kuleta maguezi , baada ya kuzembea kwa muda mrefu shule zimechukua hatau nyingi kwa pamoja. Kwa mfano zimeanzisha mitihani ya pamoja na mitihani ya kuwahamasisha watoto-mhariri anasema hayo yote yamefanyika bila ya kubadili mpango wa masomo, bila ya kuongeza walimu na bila ya kupunguza idadi ya watoto madarasani. Gazeti linasema badala ya kusaidia, mageuzi hayo yamegeuka kuwa shinikizo kwa watoto.
Na matokeo yake ni kwamba theluthi moja ya watoto wanahitaji-tuishen,yaani msaada maalum.