Magazetini.
17 Juni 2008Magazeti ya Ujerumani leo yanazungumzia juu ya mustakabali wa Ulaya, baada ya wananchi wa Ireland kuupinga mkataba wa Lisbon katika kura ya maoni.
Magazeti hayo pia yanatoa maoni juu ya uamuzi wa Saudi Arabia kuongeza uzalishaji mafuta kwa kiasi cha lita zaidi ya milioni 31 kwa siku.Jee kimetokea nini kwa wasaudia?
Tatizo la ulevi wa kupindukia miongoni mwa vijana wa Ujerumani pia linazingatiwa na wahariri katika safu zao za maoni.
Kuhusu mustakabal wa Umoja wa Ulaya baada ya kura ya maoni nchini Ireland, gazeti la Westdeutsche Zeitung linauliza jee mradi wa watu milioni mia tano uanguke kwa sababu ya kura za wachache?
Lakini mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba swali hilo linaulizwa hasa na wale wanaofahamu fika kwamba mradi huo yaani mkataba wa Lisbon ni uzuri wa mkakasi! Kilichomo ndani ni kipande cha mti. Gazeti linaeleza kuwa watu wa Ireland wameupinga mkataba huo kwa sababu hawakuelewa, maudhui yake- yumkini hayo ni kweli, lakini wananchi hao wanapambana na hali halisi ya kila siku inayotokana na maamuzi yanayopitishwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya.
Na gazeti la Braunschweiger Zeitung linaongeza kwa kusema kuwa matokeo ya kura ya maoni nchini Ireland ni ishara ya onyo.
Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa uamuzi watu wa Ireland kuupinga mkataba wa Lisbon maana yake, ni kuwa serikali za nchi za Umoja wa Ulaya zinapaswa kutekeleza siasa zitakazokuwa karibu na wananchi wao.
Na gazeti la Döbelner Anzeiger linasema, watu barani Ulaya wanataka, ajira,usalama wa kijamii, uhuru zaidi mipakani, na bei zilizotengemaa.
Mhariri wa gazeti la Bild Zeitung ameshangazwa na uamuzi wa Saudi Arabia juu ya kuongeza uzalishaji mafuta.
Wasaudia wamesema wataongeza lita milioni 31 na laki nane kila siku ili kujaribu kuteremsha bei ya mafuta duniani. Mhariri wa gazeti hilo anauliza jee kimetokea nini? Mhariri anakumbusha nasaha za aliekuwa waziri wa uchumi wa Ujerumani mnamo miaka ya 60 aliyesema kuwa ,mtu lazima kwanza amlishe ng'ombe kabla ya kumkamua maziwa. Kila mwuuza duka anajua kwamba anapaswa kuwahudumia vizuri wateja wake ili warudi tena.
Gazeti linauliza jee ,Saudi Arabia itapata faidi gani ikiwa bei ya mafuta itaendelea kuwa kubwa na kulazimisha watu wauze magari yao?
Maoni ya gazeti la Nordwest Zeitung yanahusu ulevi wa kupindukia miongoni mwa vijana nchini Ujerumani.
Gazeti linatilia maanani kuwa mnamo kipindi cha miaka mitano idadi ya vijana wanaopelekwa hospitilani kutokana na tatizo la ulevi wa kutopewa-imeongezeka mara mbili.
Gazeti linasema, tofauti na bei ya mafuta ,bei ya pombe ni ya chini nchini Ujerumani.
Kutokana na hayo itakuwa vigumu kuwalinda vijana. Kwani sheria peke yake haitoshi.