Magazetini
6 Agosti 2008Katika maoni yao wahariri wamagazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya
mabilioni ya fedha zinazotumika kwa ajili ya silaha wakati ni kiasi kidogo tu kinatumika kwa ajili ya kupiga vita maradhi kama ukimwi.
Gazeti la Morgenpost linasema yumkini watu wataweza kutoa pumzi ya faraja kutokana na bei ya mafuta kuanza kupungua.
Magazeti ya Pforzheimer na Wetzlarer Neue Zeitung yanalalamika juu ya usuhuba unaofanyika kwenye Umoja wa Ulaya inapohusu kuajiri wafanyakazi.
Juu ya fedha nyingi zinazotumika kwa ajili ya silaha badala ya kutumia fedha hizo kwa ajili ya kupambana na maradhi gazeti la Braunschweiger linasema kuwa binadamu amepoteza maadili ya mshikamano. Ni jambo linalotia uchungu kuona kuwa miradi mingi inayohusu maradhi ya ukimwi haiendi sambamba na shabaha za kijamii.
Gazeti linasema fedha nyingi sana zinatumika kwa ajili ya silaha duniani wakati ni kiasi kidogo tu kinachotolewa kuwasaidia watu wanaougua maradhi ya ukimwi. Gazeti la Braunschweiger linatilia maanani kwamba nchini Uhispania pameanzishwa shirika la misaada la wasanii wasiojali mipaka. Wasanii hao wanawatumbuiza pia watoto wenye ukimwi,ili kuwafariji watoto hao.
Mhariri wa gazeti hilo ,anasema litakuwa jambo la manufaa makubwa ikiwa wasanii hao watatumbuiza mbele ya wanasiasa ili wanasiasa hao watahayari.
Gazeti la Berliner Morgenpost linasema yumkini watu wameshakivuka kipindi kigumu cha bei ya mafuta
Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa nchi zinazozalisha mafuta za shirika la OPEC hazitapata manufaa yoyote ikiwa bei ya mafuta itaendelea kupanda. Kupanda huko kwa bei kunaathiri ustawi wa uchumi wa dunia.
Mhariri wa gazeti la Berliner Morgenpost anatilia maanani kwamba hata mwenyekiti wa shirika la OPEC angependelea kuona bei ya mufuta ikiteremka hadi kufikia dola 80 kwa pipa moja. Gazeti linasema hayo yanaonesha kuwa dunia imeshavuka kipindi kigumu katika bei ya mafuta.
Gazeti la Wetzlarer Neue Zeitung linalalamika kuwa wanasiasa kwenye Umoja wa Ulaya wanaajiri ndugu zao na kuwalipa mishahara inayotokana na fedha za walipa kodi. Jambo la kushangaza ni kwamba hadi sasa wamekuwa wanaruhusiwa kufanya hiyvo. Lakini sasa baraza la bunge la Umoja huo linataka kukomesha utaratibu huo.