Magazetini.
7 Mei 2009
Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya mkataba mpya wa Umoja wa Ulaya na juu ya mazoezi ya kijeshi yanayofanywa na nchi za Nato nchini Georgia .
Mkataba wa Umoja wa Ulaya-unaoitwa mkataba wa Lisbon unapaswa kuidhinishwa na nchi zote wanachama wa Umoja huo ili uweze kutumika. Lakini pamekuwa na mashaka mashaka miongoni mwa wanachama fulani.
Hatahivyo gazeti la Darmstädter Echo linasema Umoja wa Ulaya ungali hai!
Mhariri wa gazeti hilo anasema katika maoni yake kwamba Umoja wa Ulaya bado ungali hai- kwa sababu bunge la nchi Jamhuri ya Czech limeukubali mkataba huo wa mageuzi.
Mhariri huyo anatilia maanani kwamba Jamhuri ya Czech iilikuwa miongoni mwa nchi zilizokuwa zinayumbayumba kuhusu mkataba huo.
Na mhariri wa gazeti la Münchner Merkur anasema hatua ya seneti ya Jamhuri ya Czech kuukubali na kuupitisha mkataba huo angalau katika seneti, ni ishara ya matumaini.
Gazeti hilo linasema licha ya kasoro na maswali mengi yaliyopo juu ya mkataba wa Lisbon, uamuzi wa seneti ya Jamhuri ya Czech umekuja wakati mujarab-kwani ni hatua inayoashiria kuondokana na taasisi zinazojikwamishwa zenyewe ndani ya Umoja wa Ulaya. Gazeti la Münchner Merkur linatilia maanani kwamba wananchi zaidi na zaidi katika nchi za Umoja wa Ulaya wanatambua umuhimu wa bara lao katika kuwa na uwezo wa kuchukua hatua, kama jinsi inavyoonekana sasa katika nyakati za mgogoro wa uchumi unaoikabili dunia.
Gazeti la Financial Times Deutschland pia linazungumzia juu ya mkataba wa Lisbon kwa kuipongeza Jamhuri ya Czech kwa hatua iliyochukua ili kulisogeza mbele bara la Ulaya.
Gazeti la Westdeutsche Zeitung linazungumzia juu ya mazoezi ya kijeshi ya nchi za Nato nchini Georgia.
Mhariri wa gazeti hilo anasema kuwa licha ya upinzani na shutuma za Urusi mazoezi hayo yaliyoanza jana nchini Georgia, lazima yaendelee kufanyika la sivyo Nato itavurugika wajihi.