Adhabu ndogo kwa Aung San Suu Kyi ni ushindi kwa jumuiya ya kimataifa!
12 Agosti 2009Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya hukumu iliyotolewa kwa kiongozi wa upinzani nchini Myanmar Aung San Suu Kyi na hukumu nyingine iliyotolewa nchini Ujerumani kwa aliekuwa kamanda katika jeshi la Ujerumani wakati wa vita kuu. Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya mkutano mkuu wa chama cha wapalestina Fatah.
Kama ilivyokuwa inahofiwa na jumuiya ya kimataifa, kiongozi wa upinzani nchini Myanmar San Suu Kyi ameongezewa adhabu na watawala wa kijeshi wa nchi hiyo.
Jana mahakama ilimhukumu mwanasiasa huyo kifungo cha miaka mitatu jela ,lakini adhabu hiyo imebadilishwa, na badala yake ameongezewa miezi 18 ya kifungo cha nyumbani.
Juu ya hukumu hiyo mhariri wa gazeti la Nürnberger Nachrichten anasema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuitathmini adhabu hiyo ndogo kuwa ni mafanikio ya kampeni yake. Gazeti hilo linasema sasa halitakuwa jambo la manufaa kutoa miito juu ya kuimarisha vikwazo dhidi ya watawala wa Myanmar. Sababu ni kwamba biashara kati ya nchi za Umoja wa Ulaya na Myanmar ni ndogo sana kiasi kwamba vikwazo hivyo havitakuwa shinikizo kwa watawala hao.
Na gazeti la Badische Neueste Nachrichten linasema hukumu iliyotolewa kwa San Suu Kyi inaonyesha kwamba utawala wa Myanmar bado upo mbali sana na demokrasia.
Na nchini Ujerumani mahakama ya mjini Munic jana ilitoa adhabu ya kifungo cha maisha kwa aliekuwa kamanda katika jeshi la mafashisti wa Kijerumani. Mtu huyo Josef Scheungraber- mwenye umri wa miaka 90 alipatikana na hatia ya kuamrisha mauaji halaiki kwenye kijiji kimoja nchini Italia,wakati wa vita kuu.
Juu ya hukumu hiyo gazeti la Allgemeine Zeitung linasema, ni muhimu, na pia ni lazima sana, kutoa adhabu hiyo, hata kama uhalifu ulitendwa miaka 40 iliyopita.
Gazeti hilo linasisitiza kuwa jambo muhimu ni kwamba haki imetendeka kwa niaba ya wahanga na kwa ndugu na jamaa wa wahanga hao.
Gazeti la Sächsiche Zeitung pia linazungumzia juu ya adhabu ya fashisti huyo kwa kueleza kwamba adhabu aliyopewa mtu huyo Scheungraber siyo kashfa, asilani kama anavyodai wakili wake.Gazeti linaeleza kuwa tunachoweza kusema kuwa kashfa ni kwamba hukumu hiyo imetolewa baada ya miaka 40 au 50. Mhariri wa gazeti la Sächsiche Zeitung anasema kuchelewa kutolewa kwa adhabu hiyo kunaonesha ni kwa kiasi gani , ilikuwa vigumu, baada ya kumalizika vita kuu vya pili , kwa idara za sheria za Ujerumani kufuatilia uhalifu uliotendwa na utawala wa mafashisti.
Gazeti hilo linatahadharisha kuwa ,kila mwaka unavyopita ndivyo inavyokuwa vigumu kuthibitisha uhalifu wa mafashisti kwa sababu mashahidi muhimu wameshakufa siku nyingi.
Gazeti la Stuttgarter Zeitung linazungumzia juu ya mkutano mkuu wa chama cha wapalestina, Fatah.
Gazeti hilo linawaambia wapalestina kuwa sasa umefika wakati wa kuachana na mkakati wa kutumia mabavu,kwa sababu makakati huo hautafua dafu mbele ya Israel.
Mwandishi/Mtullya Abdu.
Mhariri/Abdul-Rahman