1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Karua: Kinachoendelea Tanzania sio uchaguzi

29 Oktoba 2025

Wadau wa kikanda wa kutetea haki wanatiwa wasiwasi na hali nchini Tanzania ambako uchaguzi mkuu unafanyika. Wakati huohuo, waandishi wa kigeni kutokea nchi jirani wamekumbana na vikwazo vya usajili vilivyowaacha nje.

Uchaguzi wa Tanzania 2025
Kiongozi wa chama cha PLP Martha Karua Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Kwenye taarifa yao ya pamoja na washirika wa kikanda chini ya mwamvuli wa Jumuiya ni Yetu, tume ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya- KHRC- imetahadharisha kuwa mazingira yaliyopo hayaruhusu uchaguzi kufanyika kwa uhuru na haki. Martha Karua ni kiongozi wa chama cha PLP ambacho ni mwanachama wa muungano huo wa kikanda na anasisitiza kuwa kinachotekea Tanzania sio uchaguzi na,”Ili uchaguzi uwe wa huru na haki, sharti kuwe na ushindani. Huu sio uchaguzi kwani hakuna wagombea wa upinzani. Kwa hiyo ni maigizo au mchezo wa kuigiza.”alisistiza.

Tume ya KHRC imeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ilivyo ya haki za binadamu na uhuru wa kisiasa ukizingatia malengo ya Jumuiya.

"Kwa mtazamo wao, taarifa yao imekashifu vitendo vinavyowanyima haki na uhuru wagombea wa upinzani kushiriki kwenye uchaguzi mkuu. Leonard Onyango ni mkaazi wa Nairobi na amekuwa akifuatilia siasa za Tanzania kwa muda na anahisi kuwa katiba inahitaji kufanyiwa kazi kwani, ”Uchaguzi wa Tanzaniaunaonyesha jinsi ambavyo demokrasia imedidimia. Siwalaumu walioko madarakani ila nainyoshea kidole katiba iliyo na mapungufu.Nikitazama uchaguzi wa Kenya huwa una ushindani mkali lakini ni tofauti kwa Tanzania.”

Waangalizi wa kimataifa walijiondoa

Wakinukuu taarifa na utafiti wa hivi karibuni wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, tume ya KHRC imedai kuwa hali imewabana zaidi wahusika hata waangalizi wa kinataifa wamejiondoa kwenye zoezi hilo. Duru zinaeleza kuwa Ubelgiji, Sweden, Ireland na Ujerumani hawajapeleka waangalizi wao, na kwamba shirika la Umoja wa mataifa la maendeleo, UNDP, pia halijawakilishwa safari hii.

Picha: Jeremy Chan/Getty Images

Taarifa hiyo pia imetiwa wasiwasi na vikwazo vilivyowekewa vyombo vya habari na majukwaa ya mitandaoni kwani mashirika ya habari ya kimataifa yamepigwa marufuku kuingia Tanzania na vibali kufutiliwa mbali. Boniface Mwangi ni mwandishi wa habari na mtetezi wa haki nchini Kenya na aliwahi kujikuta pabaya alipoizuru Tanzania kusimama na kiongozi wa chama cha upinzani cha CHADEMA Tundu Lissu anayezuiliwa jela kwa uhaini.

Kwa mtazamo wake uchaguzi huu hauna mashiko kwani, ”Uchaguzi huu ni kati ya Suluhu na Samia. Sijaona mpinzani wake yeyote.Kama jumuiya ya Afrika Mashariki tunawaombea raia wa Tanzania...tunajua kwamba hakuna uchaguzi leo.Ni kupoteza wakati tu.”anasimulia.

Tuzo ya DUA

Yote hayo yakiendelea,kiongozi wa upinzani wa CHADEMA Tundu Lissu na mwenzake wa Uganda Kizza Besigye ambao wanazuiliwa jela katika nchi zao wametambuliwa kama mabingwa wa demokrasia barani Afrika na kongamano la mwaka huu la Umoja wa Demokrasia barani Afrika.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW