Maoni yanatofautiana katika kuitambua au la serikali mpya ya Palastina
18 Machi 2007Jerusalem:
Baraza la mawaziri la Israel limeitika mwito wa waziri mkuu Ehud Olmert wa kuisusia serikali mpya ya Palastina.Mawaziri wawili tuu kati ya 21 wameupinga mwito huo.Waziri mkuu Ehud Olmert anahoji ametoa mwito huo baada ya serikali ya umoja wa taifa ya Hamas na Fatah kukataa kuachana na matumizi ya nguvu na kutoitambua Israel pia.Hata hivyo waziri mkuu Ehud Olmert ameahidi ataendeleza mawasiliano pamoja na rais Mahmoud Abbas.Ujerumani,mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa ulaya,imesema Umoja huo utasubiri kuona vitendo vya serikali mpya kabla ya kuamua kuipatia upya misaada serikali hiyo.Ofisi ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini Jerusalem imesema Marekani itawasiliana na mawaziri wasio wa Hamas tuu,tena chini ya misingi maalum.Norway imeshasema itaitambua serikali mpya.Nazo Urusi na Ufaransa zinasema zitashirika na serikali hiyo inayoongozwa na Ismael Hanniyeh.Baraza jipya la mawaziri la palastina linakutana kwa mara ya kwanza hii leo.