1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni:Mashamba madogo ndiyo mustakabali wa mifumo ya chakula

Sabrina Elba26 Julai 2021

Wakulima wadogo wanaweza kutoa mchango mkubwa katika kujenga mifumo endelevu ya chakula. Lakini uwekezaji zaidi unahitajika, anaandika Sabrina Elba, balozi wa hisani wa mfumo wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo.

Dürre im Süden Angola
Picha: Adilson Abel/DW

Miaka miwili iliyopita mimi na mume wangu tulikwenda Sierra Leone ambako tulikutana na watu jasiri. Watu hao, akina mama na akina baba waliweza kuhimili misukosuko ya vita viliyvoikumba nchi yao na pia athari za janga la Ebola, lakini walisonga mbele na maisha yao.

Matumaini yalionekana wazi na mustakabal ulikuwa wa matarajio makubwa. Kabla ya hapo hakuna aliyekuwa anajua kwamba janga jingine lilikuwa njiani la maambukizi ya virusi vya corona.

Hata hivyo ukweli ni kwamba hata kabla ya janga hilo, nchi nyngi za Afrika kwa miezi mingi zilizikuwa zinakabiliwa na matatizo makubwa. Nchi kadhaa, ikiwa pamoja na Zimbabwe zilikuwa zinapambana na athari za ukame mbaya kabisa kuwahi kutokea katika kipindi cha miongo kadhaa. 

Nchi za eneo la mashariki mwa Afrika nazo zilikumbwa na baa la nzige walioteketeza mazao. Hali hiyo ilikuwa haijatokea kwa kipindi cha miaka 70. Baa la nzige lilizidisha umasikini na lilihatarisha mfumo wa upatikanaji wa chakula kwenye eneo hilo.

Ziara yetu nchini Sierra Leone ilinifunza kitu kimoja, kwamba binadamu wanaweza kuhimili shida: Iwe ni vita, majanga ya asili au maambukizi ya virusi, binadamu wanaweza kuzikabili shida hizo, mradi tu wanapatiwa msaada stahiki.

Sabrina Elba anaufanyia kazi mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo.Picha: privat

Katika ziara hiyo niliweza kujifunza juu ya nguvu ya kilimo. Jinsi kilimo kinavyochepua maendeleo ya kilimo na kijamii. Niliweza kutambua kwamba, ikiwa tunataka kuwawezesha akina mama na vijana na ikiwa hasa tunajali umuhimu wa ardhi na dunia yetu, tunapaswa kuwathamini watu wanaopanda mazao yaani wakulima wadogowadogo kwani wao ndiyo walinzi wa sayari yetu ya dunia.

Wakulima hao wanatoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa chakula wa uhakika. Wanazalisha  asilimia 30 ya chakula chote duniani. Dhima yao ni kubwa zaidi katika nchi za kusini ya jangwa la Sahara ambako wanazalisha asilimia 80 ya chakula chote kinachopatikana kwenye eneo hilo.

Madogo kumuundo, lakini manufaa makubwa

Duniani kote mashamba milioni 500 ya wakulima wadogowadogo yanazalisha chakula kwa ajili ya watu zaidi ya bilioni 2. Mashamba ni madogo lakini manufaa yake ni makubwa.

Hata hivyo wakulima hao wanaishi kwenye maeneo yaliyomo katika hatari kubwa ya kukumbwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Ikiwa hawatapatiwa msaada, maafa yanaweza kuwa makubwa kwenye jumuiya zao na katika mfumo wa chakula duniani kwa kutilia maanani kwamba wao ndiyo nguzo ya mfumo huo.

Wakulima wadogowadogo wanakabiliwa na changamoto kadha wa kadha, ikiwa pamoja na jukumu la kukidhi mahitaji ya binadamu wanaoongezeka. Pia wanakabiliwa na tatizo la kupungua kwa mazao wanayozalisha kutokana na kuharibika kwa ardhi inayoweza kulimika. Pamoja na hayo pana tatizo la ongezeko la joto linaloweza kusababisha kupungua kwa mazao kwa asilimia 25.

Upo ulazima wa kuwawezesha wakulima hao wa  sehemu za mashambani,kwa kuwapa mbinu za kuzikabili changamoto zinazotokana na ugeu geu wa hali ya hewa. Ni kwa njia hiyo kwamba itawezekana kuhakikisha uthabiti wa maendeleo barani Afrika.

Afrika inao uwezo wa kuilisha dunia, ikiwa msaada stahiki utapatikana. Maendeleo ya kilimo barani Afrika yanatia moyo. Uzalishaji umeongezeka kwa asilimia 160 katika kipindi cha miaka 30 iliyopita na hivyo kuvuka  kiwango cha wastani wa dunia. Hata hivyo bado pana haja ya maboresho. Hadi sasa ni asilimia 1.7 tu ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya dharura za tabia nchi zimekwenda kwa wakulima wadogowadogo. 

Ikiwa nchi zitachukua hatua sasa na kutekeleza ahadi zilizotoa za msaada wa fedha kwa ajili ya juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi zitakuwa zinawekeza katika maendeleo ya siku za usoni.

Chanzo:DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW