1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni:Uhuru wa kutoa maoni hauna mjadala

Josephat Nyiro Charo8 Januari 2015

Shambulizi la Paris litauchochea zaidi mjadala kuhusu Uislamu na wakimbizi barani Ulaya. Lakini mwandishi wa DW Christoph Haselbach anasema uhuru wa kutoa maoni na kuvumiliana si masuala ya kufanyiwa mzaha.

Frankreich Anschlag auf Charlie Hebdo - Screenshot charliehebdo.fr
Picha: charliehebdo.fr

Shambulizi la Paris halikufanyika bila kutarajiwa. Jarida la Charile Hebdo tayari mwaka 2006 lilichapisha katuni za mtume Mohammed zilizokuwa zimetolewa awali na gazeti la Denmark Jyllands Posten na kuibua ghadhabu miongoni mwa Waislamu ulimwenguni kote. Wakati huo kulifanyika mashambulizi kadhaa katika mataifa ya kiislamu dhidi ya taasisi na wakala za Denmark na nchi nyingine za magharibi. Mwaka 2011 kukafanyika shambulizi dhidi ya ofisi za Charlie Hebdo jijini Paris.

Hayo yote hayakulizuia jarida hilo kuchapisha vibonzo vya kumbeza mtume Mohammed na Uislamu: Miongoni mwa mambo mengine yaliyoanzishwa na jarida hilo ni toleo maalumu kuhusu Sharia, likisimamiwa na mhariri mkuu aliyejulikana kama Mohammed. Pia si sadfa kwamba ukurasa wa mbele wa toleo la hivi karibuni la jarida hilo lilikuwa na picha ya Michel Houllebecq, mwandishi ambaye amechapisha kitabu chenye utata mkubwa ambacho kinaionyesha Ufaransa ikitawaliwa na rais muislamu.

Waislamu wachukuliwe kama watu wengine

Je jarida linaruhusiwa kufanya mzaha kuhusu dini na mitume wake? Bila shaka linaweza kwa mujibu wa sheria za nchi. Jarida la Charlie Hebdo mara kwa mara limefanya mizaha kuhusu kiongozi wa kanisa katoliki na kushinda kesi mahakamani baada ya kushtakiwa na shirika moja la kanisa hilo. Wakristo wa kanisa Katoliki wanakerwa sana na vibonzo vya kiongozi wao, lakini wanaikubali hali hiyo na kuivumilia.

Hata serikali hairuhusiwi kuingilia suala hili. Katika uamuzi sahihi mwaka 2006 waziri mkuu wa Denmark wakati huo Anders Fogh Rasmussen, alikataa miito ya waislamu kote ulimwengu kumtaka achukue hatua za kisheria dhidi ya katuni za kinafiki zilipochapishwa nchini humo wakati huo. Jamii huru yenye demokrasia lazima iyavumilie mambo hayo. Na nchi lazima itarajie uvumilvu huu kutoka kwa raia wake wote. Haiwezekani kuwa na mfumo maalumu wa kuwashughulikia waislamu.

Wasiwasi wazidi kuongezeka

Kufuatia shambulizi baya namna hii kuna majaribu ya kuhimiza kuwepo utulivu. "Acheni kutia chumvi, nyie mnaotumia vibonzo kufanya mzaha kuhusu Uislamu tafadhili acheni sasa. Hatutaki vita vya kidini." Lakini hilo lingekuwa jambo ambalo hasa magaidi wanalitaka - kuubana uhuru kwa hiari. Mbinu hii ya usaliti kupata kitu kwa kutumia nguvu haistahili kuruhusiwa ifaulu.

Mwandishi wa DW, Christoph HasselbachPicha: DW/M.Müller

Lakini inatia wasiwasi kufikiria kuhusu kitakachotokea baada ya hujuma hii. Wasiwasi mkubwa ambao umekuwepo Ufaransa utaendelea kuongezeka. Nchi hiyo ina asilimia kubwa ya waislamu. Wengi hawana ajira na wanaishi katika hali ngumu katika makazi duni. Polisi hawaendi katika baadhi ya makazi hayo. Kwa upande mwingine chama cha siasa za mrengo wa kulia cha National Front hakitaki wageni na hasa kinapinga waislamu. Kilishinda uchaguzi wa Ulaya mwaka uliopita na sasa waliokipigia kura watahisi walifanya uamuzi sahihi kukichagua. Chuki dhidi ya Uislamu itaongezeka sambamba na ghadhabu miongoni mwa waislamu - mzunguko usioisha.

Baadhi wamekuwa wakifahamu

Na matokeo hayataonekana tu nchini Ufaransa. Katika karibu kila nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya vyama vinavyowachukia wageni vimeibuka katika miaka ya hivi karibuni. Vitasema: Unaona, Waislamu si wetu hawa, hawawezi kujumuishwa katika jamii." Vitendo vya watu wachache katika kundi la wachache vinatumiwa kusimamia dini yote na wafuasi wake wote. Hata nchini Ujerumani pia vuguvugu linalopinga Uislamu la Pegida litaona nchi za magharibi zinakabiliwa na kitisho cha kuenea kwa Uislamu.

Hatupaswi kujihadaa wenyewe. Kuishi pamoja kwa maelewano katika jamii hakutakuwa rahisi. Kwa hiyo ni muhimu sana kuwa na busara na kuwa macho. Ndio ni shambulizi baya kabisa dhidi ya uhuru wetu ambalo hakuna anayeweza kulihalalisha. Hatutamruhusu mtu yeyote kutupokonya uhuru wetu. Lakini vivyo hivyo lazima tusimruhusu mtu yeyote atupokonye uvumilivu wetu. Hakuna sababu kwa sisi kuwashuku waislamu wote au kutilia shaka mtindo wa kuishi pamoja kwa amani.

Mwandishi:Josephat Charo/Hasselbach, Christoph

Mhariri:Daniel Gakuba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW