1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni:Umoja wa Mataifa umeshindwa

23 Septemba 2016

Mvutano kati ya Marekani na Urusi kuhusu vita nchini Syria kufuatia mashambulizi dhidi ya msafara wa magari ya msaada unadhihirisha kushindwa kwa Umoja wa Mataifa

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New-York
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New-YorkPicha: Reuters/E. Munoz

Kwa hakika Umoja wa Mataifa umefikia kikomo.Mfumo wa taasisi hiyo muhimu ya dunia umeshapitwa na wakati na hauendani tena na hali halisi ya dunia ya sasa ambapo mizozo haizingatia mipaka ya mataifa, na ambapo kipaumbele ni kueneza itikadi badala ya kukamata maeneo. Kwa mivutano na malumbano kama iliyoshuhudiwa kati ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov hata ulimwengu umejidhihirishia wenyewe jinsi hali ilivyoshindikana.Kwa maana hiyo chombo hicho kinachoongozwa kwa urasimu mkubwa kimeonekana wazi kwamba hakiwezi kuisaidia Syria wala wasyria wenyewe.

Mashambulizi ya mabomu dhidi ya msafara wa magari ya msaada uliokuwa ndio matumaini makubwa kwa maelfu ya watu nchini Syria, ni kitendo kibaya zaidi ambacho kimeudhihirishia ulimwengu kwamba mazungumzo na makubaliano yaliyofikiwa juu ya kusitisha vita hayakuleta tija yoyote,na badala yake watu wanaendelea kufa,usiku na mchana na hata wakati huu ninapoisoma tahariri hii.

Ulimwengu ulikuwa tafauti kabisa wakati Umoja huo wa Mataifa ulipoasisiwa mwaka 1945 wakati huo katika mazingira ya madhara ya vita vikuu vya pili vya dunia. Na kwa maana hiyo Umoja wa Mataifa uliundwa kwa kuzingatia hali hiyo lengo likiwa ni kuzuia vita kama hivyo visijirudie. Nchi zinazounda taasisi hiyo hazina nguvu lakini badala yake nchi tano wanachama wa kudumu katika baraza la usalama la Umoja huo ndio waliopewa nguvu zote kwa kushikilia kura ya turufu.

Matokeo ya hilo ni kwamba nchi zenye nguvu kiuchumi kama Brazil na India hazina sauti yoyote katika chombo hicho na kama haitoshi hata nchi kama Ujerumani yenye uzoefu mkubwa katika vita vya dunia haishikiliii nafasi yoyote katika chombo hicho tangu mwaka 1973. Mfumo wa taasisi hiyo haujabadilika sana toka ilipoundwa,kinachoshuhudiwa hadi sasa ni kwamba nchi kama Urusi au China au Marekani zinaweza bila matatizo yoyote kuzuia uamuzi wa aina yoyote ndani ya chombo hicho kwa kutumia mamlaka ya kura ya Turufu.Hata suala la nani atashikilia wadhifa wa kukiongoza chombo hicho kama katibu mkuu unaamuliwa na nchi hizo.

Mwandishi wa DW Ines PohlPicha: DW

Muundo wa chombo hicho pia unazuia mtu yoyote mwenye mtazamo wa kuleta mageuzi makubwa kuchaguliwa kuiongoza taasisi hiyo awe mwanamme au mwanamke.Na matokeo yake siku zote anayechaguliwa anabidi kuwa mtu atakayeliweza jukumu la kuurudhisha kila upande na asiyeweza kuthubutu kuyagusu masuala tete yanayozigusa nchi hizo.Taasisi ambayo umuhimu wake unahitajika kuonekana hususan wakati huu ambapo ulimwengu unakabiliwa na tatizo kubwa la ugaidi inajikuta ikiwa katika hali ya mtengano baina ya mataifa na kupoteza uthabiti wa kimuundo na kushindwa hata kuwa na ushawishi au nguvu za kujiokoa yenyewe.

Yote hayo ni kwasababu pengine nchi hizo zinazoshikilia madaraka ya Umoja huo ambazo ni zile zilizokuwa na nguvu katika vita vya pili vya dunia hazijatambua kwamba peke yao hawawezi kuipatia ufumbuzi migogoro kama ya Syria na wanachotakiwa kukifanya ni kuwaachia wengine washike usukani ili Umoja wa Mataifa unaozishirikisha nchi zote usimame kuwa chombo imara cha kuleta maridhiano katika Ulimwengu.

Na kwa mivutano na uhasama katika uhusiano wa nchi kama Marekani na Urusi ni wazi kwamba hilo la kufanyika mageuzi ya kimuundo kwenye chombo hicho halitowezekana katika kipindi cha hivi karibuni,licha ya kwamba hata viongozi kama rais wa Marekani Barack Obama ameshatambua kwamba ipo haja ya mageuzi ya kimuundo kutokea katika Umoja huo ili kuendana na changamoto mpya za ulimwengu huu.Nchi zenye nguvu zinapaswa kutambua kwamba haziwezi tena kushinda bila ya kutambua changamoto hizi mpya za ulimwengu huu.

Mwandishi:Ines Pohl/Saumu Mwasimba

Mhariri: Daniel Gakuba

LINK: http://www.dw.de/dw/article/0,,19569434,00.html