Maonyesho ya compyuta CeBIT
2 Machi 2009Mwaka huu pirikapirika zimepunguka katika maonyesho ya Cebit.Hata kwenye uwanja wa kuegeza magari hakuna msongamano-unaweza kuliegeza gari lako karibu na mlango wa kuingilia kumbi za maonyesho.Kuna nafasi za kutosha kuegeza magari-mwaka huu kumbi mbili zimebakia tupu. Juu ya hivyo,msemaji wa CeBIT Hartwig von Saß anashukuru kuwa mambo si mabaya kama ilivyokuwa ikihofiwa.
Anasema,mwaka huu makampuni 4,300 kutoka nchi 69 yanashiriki katika maonyesho makubwa kabisa ya compyuta duniani-CeBIT.Hiyo bila shaka ni idadi ndogo kulinganishwa na miaka iliyopita.Lakini von Saß anaamini kuwa hayo ni mafanikio makubwa hasa wakati huu ambapo ulimwengu mzima unapambana na uchumi ulioporomoka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushudiwa tangu miaka 70 iliyopita.
Hasa makampuni madogo dogo kutoka nchi za Asia ndio hazikuwakilishwa mwaka huu kwenye maonyesho ya CeBIT.Si kwa sababu ya mzozo wa uchumi tu bali yametoweka kabisa.Hayo ni matokeo ya mashindano ya kufa kupona katika masoko ya dunia. von Saß anaeleza hivi:
"Hapo kilicho muhimu ni kuwa makampuni makubwa yaliyo kama uti wa mgongo wa IT yaani teknlojia ya mawasiliano kote duniani, yamewakilishwa katika maonyesho ya CeBIT mwaka huu vile vile.Hayo ni makampuni kama vile IBM,SAP,Microsoft na mengi mengine yaliyo kiini cha biashara ya IT."
Hata hivyo,maonyesho ya CeBIT hayakuathirika tu kutokana na msukosuko wa kiuchumi sawa na wote wengine.Mashindano makali yamemegua sehemu ya biashara yake.Kwa mfano,takriban makampuni yote ya vyombo vya elektroniki katika sekta ya burudani yamehamia Berlin kwenye maonyesho ya redio na televisheni na makampuni ya simu za mkono pia yamekimbilia maonyesho yanayofanywa Barcelona nchini Uhispania.
Kwa maoni ya msemaji wa CeBIT, kilicho muhimu sana hivi sasa wakati ambapo ulimwengu unakabiliwa na uchumi uliodorora, ni kushughulikia biashara kwani makampuni 4,300 yanayowakilishwa Hannover yana matumaini makubwa kupata biashara mpya itakayosaidia kuyatoa makampuni hayo katika mgogoro wa sasa wa kiuchumi haraka iwezekanavyo.