Maonyesho ya kilimo yafunguliwa kwa umma mjini Berlin
18 Januari 2008Wiki ya 73 ya maonyesho ya kimataifa ya kilimo imefunguliwa rasmi kwa raia mjini Berlin hii loe. Waziri wa kilimo wa Ujerumani,Horst Seehofer, kama desturi ameyatembelea maonyesho hayo.
Zaidi ya washirika 1,600 kutoka nchi 52 wanaonyesha bidhaa zao katika maonyesho hayo ya siku kumi.
Jana, siku ya kwanza ya maonyesho hayo, ilikuwa siku ya wanasiasa na wataalamu wa viwanda, mada kuu ikiwa nyama kutoka kwa wanyama wanaozalishwa kutumia mbegu zilizohifadhiwa kwenye mahabara.
Waziri Seehofer amesema nyama hiyo haitaruhusiwa kuuzwa katika masoko ya hapa Ujerumani.
Muungano wa wakulima wa Ujerumani wamekubaliana na kauli ya idara ya chakula na dawa ya Marekani iliyosema nyama kutoka kwa wanyama wanaozalishwa kutumia mbegu za wanyama zilizohifadhiwa kwenye mahabara ni chakula salama cha binadamu.