1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mapambano kuwania jimbo la Panjshir yaendelea Afghanistan

5 Septemba 2021

Kundi la Taliban na vikosi vya wapiganaji pinzani wamekabiliana siku nzima ya Jumamosi kudhibiti jimbo la Panjshir kaskazini mwa mji wa Kabul, eneo la mwisho nchini Afghanistan kutoa upinzani mkali dhidi ya Taliban.

Afghanistan, Panjshir | Widerstandskämpfer gegen die Taliban bei einem militärischen Training
Mapambano kwenye jimbo la Panjshir Picha: Jalaluddin Sekandar/AP/picture alliance

Pande zote mbili zimedai kuwa zinalidhibiti eneo la juu la bonde la Panjshir lakini hakuna upande wowote uliweza kutoa ushahidi wa hilo.

Kundi la Taliban, ambalo limefanikiwa kuchukua udhibiti wa karibu nchi nzima wakati vikosi vya kigeni vilipokusanya virago na kuondoka Afghanistan, halikuweza kulitawala eneo la Panjshir lilipokuwa likiiongoza Afghanistan kuanzia mwaka 1996 hadi 2001.

Msemaji wa Taliban Bilal Karimi amearifu kuwa wilaya za Khinj na Unabah zimekamatwa hatua iliyowezesha wapiganaji wa Taliban kuchukua udhibiti wa wilaya nne kati ya saba za jimbo la Panjshir.

"Wapiganaji wa Taliban wanasonga mbele kuelekea katikati mwa jimbo hilo" aliandika Karimi kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Wapiganaji pinzani wapinga madai ya Taliban kupata ushindi

Wanawake wa Afghanistan waandamana kudai haki zaoPicha: Bilal Guler/AA/picture alliance

Hata hivyo kundi la wapiganaji wa National Resistance Front of Afghanistan wanaomtii kiongozi wa eneo la Panjshir Ahmad Massoud limesema kuwa limewazingira "maelfu ya magaidi" kwenye ujia wa Khawak na kwamba wapiganaji wa Taliban wameyatelekeza magari na vifaa vingine kwenye eneo la Dashte Rewak.

Msemaji wa kundi hilo pinzani Fahim Dashti amezungumzia kile amekiita "mapambano makali" kuwa yanaendelea.

Kupitia ujumbe kwenye ukurasa wa Facebook, Massoud amesisitiza kuwa Panjshir "inaendelea kusimama imara". Msemaji huyo pia amewasifu wanawake waliondamana mjini Herat kudai haki zao akisema wameonesha Waafghani hawajakata tamaa kudai haki na "hawaogopi vitisho"

Mkuu wa Jeshi la Marekani aonya uwezekano wa kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe

Mkuu wa Jeshi la Marekani Mark MilleyPicha: Erin Scott/REUTERS

Wakati hayo yakijiri mkuu wa jeshi la Marekani Jenerali Mark Milley amezungumzia uwepo wa hali tete nchini Afghanistan.

"Fikra zangu za kijeshi ni kwamba hali iliyopo inaweza kuzidi makali na kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Sifahamu iwapo Taliban wataweza kuchukua udhibiti kamili na kutawala" amesema Jenerali Milley.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Fox News kutoka uwanja wa ndege wa jeshi wa Ramstein nchini Ujerumani, Milley amesema iwapo Taliban haitomudu kudhibiti hali ya mambo hilo litachochea kushamiri tena kwa makundi ya itikadi kali ikiwemo Al Qaeda au kundi linalojiita Dola la Kiislamu au makundi mengine "kigaidi" miaka mitatu inayokuja.

Wakati mapambano yakiendelea huko Panjshir, mjini Kabul shamrashamra ziliripuka baada ya kuzagaa kwa taarifa kuwa Taliban wamelikamata jimbo la Panjshir.

Mashirika ya habari ya kimataifa yameripoti kuwa risasi zilizofyetuliwa kusherehekea taarifa hizo zimewauwa watu 17 na kuwajeruhiwa zaidi ya watu 40.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW