1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano makali yaendelea kati ya Urusi na Ukraine

19 Agosti 2024

Jeshi la anga la Ukraine limesema limezuwia mashambulizi ya usiku kucha ya Urusi katika maeneo yake ikiwemo Kiev, kwa kuharibu droni 11 zilizovurumishwa nchini mwake kutoka Urusi.

Donetsk
Mapambano makali yaendelea kati ya Urusi na Ukraine Picha: Diego Herrera Carcedo/Anadolu/picture alliance

Droni hizo ziliharibiwa katika anga ya maeneo ya Mykolaiv, Cherkasy, Vinnytsia, Kyiv, Dnipropetrovsk, Kharkiv, Sumy na Donetsk, hii ikiwa ni kulingana na jeshi la anga la Ukraine kupitia ukurasa wake wa Telegram. Hadi sasa hakuna ripoti za uharibifu wa miundombinu zilizoripotiwa kufuatia shambulizi hilo.

Haya yanajiri wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akisema jana Jumapili kwamba, operesheni ya kijeshi wanayoiendeleza katika eneo la Kursk, inalenga kuunda eneo salama litakaloizuia Urusi kufanya mashambulizi nchini Ukraine.

Jeshi la Ukraine lavunja madaraja Urusi

Hii ni mara ya kwanza rais huyo wa Ukraine ameelezea nia ya mashambulizi hayo yaliyoanza Agosti 6. Awali alisema operesheni hiyo inalenga kuilinda jamii katika eneo la mpakani la Sumy kulikoshuhudiwa mashambulizi makali. Zelensky amesema ni muda sasa wa kuvunja nguvu za kushambulia za Urusi na kujibu kadri wanavyoweza mashambulizi kutoka kwa jirani yake huyo aliyeanza uvamizi nchini mwake miaka miwili na nusu iliyopita.

Ameendelea kusema kwamba Ukraine imeharibu daraja kuu mjini Kursk na kulenga jingine lililoko karibu, na kusambaratisha njia inayotumiwa na Urusi kusafirishia bidhaa zake.

Urusi haiko tayari kuingia katika meza ya mazungumzo na Ukraine

Rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: Evgenia Novozhenina/REUTERS

Huku hayo yakiarifiwa mshauri wa sera za kigeni wa rais wa Urusi Vladimir Putin, Yuri Ushakov amesema nchi yake haiko tayari kuwa na mazungumzo ya amani na Ukraine kwa sasa kufuatia mashambulizi ya taifa hilo katika eneo lake la Kursk, lakini akaweka wazi kuwa haijaondoa mezani uwezekano wa kuwa na mazungumzo hayo.

Ukraine: Urusi inaendelea kushambulia eneo la Donbas

Mwezi Juni, Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema nchi yake itavimaliza vita vya Ukraine iwapo tu Kiev itakubali kuundoa azma yake ya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO na kuikabidhi Moscow mikoa minne inayodai kuwa yake masharti ambayo Kiev iliyapuuzilia mbali.

Kauli hiyo imetolewa wakati kukiwa na ripoti kwamba wanajeshi wa majini wa Urusi wamewateka wanajeshi 19 wa Ukraine katika eneo hilo la mapigano la Kursk. Kwengineko Ulkraine imeweka tena vizuizi vya umeme huku kiwango cha joto kinachoendelea kupanda nchini humo kikiyumbisha mfumo wa nishati ambao tayari ni mbovu kufuatia mashambulizi ya Urusi. Moscow ilianza tena kushambilia mfumo huo na kuharibu nusu ya mfumo wa kutoa nishati hiyo muhimu na kusababisha baadhi ya miji kubakia bila umeme

Chanzo: afp,ap reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW