Mapambano mapya Hong Kong kupinga uhamishwaji wa wahalifu
14 Julai 2019Polisi walitumia maji yenye pilipili na virungu dhidi ya makundi madogo ya waandamanaji ambao walizuwia barabara pembezoni mwa mkutano mkubwa mwingine katika eneo la Sha Tin , wilaya ambayo iko kati ya eneo kuu la mji karibu na bandari pamoja na mpaka na China.
Waandamanaji waliofunika nyuso zao walijibu kwa kuweka vizuwizi kutokana na uzio wa chuma na mpambano na polisi wa kuzuwia ghasia ukaanza.
Hong Kong imetikiswa na zaidi ya mwezi mmoja wa maandamano ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani, pamoja na wimbi la mapabiliano tofauti ya ghasia na polisi, yaliyozushwa na sheria ambayo ingeruhusu watu kupelekwa China bara na nchi nyingine.
Mwezi uliopita, jengo la bunge lilivurugwa na mamia ya watu waliojifunika nyuso zao, waandamanaji walioongozwa na vijana katika tukio ambalo halikutarajiwa.
Mswada huo tayari umesitishwa, lakini hatua hiyo haikuweza kuzima hasira ya watu ambayo imegeuka kuwa vuguvugu pana kwa ajili ya mageuzi ya kidekrasia, haki ya kupuga kura na kuzuwia kuporomoka kwa uhuru katika mji huo wenye mamlaka yake ya ndani.
Waandamanaji pia wanadai mswada huo uondolewe kabisa , uchunguzi huru ufanyike kuhusiana na polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za mipira , wale waliokamatwa wapewe msamaha, na kiongozi ambaye hakuchaguliwa wa mji huo Carrie Lam ajiuzulu.
Mamia kwa maelfu ya waandamanaji waliandamana kupitia mtaa wa Sha Tin leo Jumapili(14.07.2019), ikiwa ni wiki ya tano mfululizo ambayo Hong Kong imeshuhudia maandamano kama hayo.
Maandamano ya ghasia
Karibu maandamano yote yamemalizika kwa ghasia kati ya polisi na baadhi ya waandamanaji wachache ambao wamekuwapo wakati wote.
"Tumeandamana mara nyingi sana lakini serikali bado haitusikilizi, na kulazimisha kila mmoja kuingia mitaani," Tony Wong , mwandamanaji mwenye umri wa miaka 24 katika maandamano hayo ya Sha Tin amelieleza shirika la bahari la AFP.
Waandamanaji wengi wanayaona maandamano hayo kama sehemu ya mapambano ya uhai wao dhidi ya kile kinachoelezwa kama kuongezeka kwa mabavu ya serikali ya China.
"Huu ni wakati hatari. Watu wa Hong Kong wanaweza kuchagua kufa ama wanaweza kuishi. Tuko ukingoni lakini kwa bahati mbaya hatukufa hadi sasa bado," amesema JoJo So , mwanamke akiwa katika umri wa miaka ya 50 ambaye alihudhuria maandamano hayo.
Beijing imeendelea kumuunga mkono kwa dhati Lam, wakiitaka polisi ya Hong Kong kumshughulikia kila mtu anayehusika katika kuvamia bunge na mapambano mengine.
Chini ya makubaliano ya makabidhiano ya mwaka 1997 na Uingereza , China iliahidi kuiruhusu Hong Kong kuendelea na uhuru wake kama mahakama huru na haki kama uhuru wa kutoa maoni.