1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano mapya Jerusalem

5 Novemba 2014

Polisi ya Israel Jumatano (05.11.2014) imepambana na Wapalestina waliokuwa wakivurumisha mawe ndani ya eneo la msikiti mtakatifu wa Al-Aqsa mjini Jerusalem.

Polisi ya Israel ikimdhibiti mlowezi wa Kiyahudi alietaka kuingia kwa nguvu eneo la msikiti wa Al-Aqsa. (30.10.2014)
Polisi ya Israel ikimdhibiti mlowezi wa Kiyahudi alietaka kuingia kwa nguvu eneo la msikiti wa Al-Aqsa. (30.10.2014)Picha: Getty Images/J. Guez

Mapambano hayo yamezuka baada ya makundi ya sera kali za mrengo wa kulia ya Kiyahudi kutangaza mipango ya kulizuru eneo hilo licha ya kuongezeka kwa mvutano uliokuweko kwa wiki kadhaa sasa.

Ziara hiyo iliopangwa na kundi la Wayahudi wakiwemo wanasiasa wa sera kali za kizalendo ilikuwa ifanyike wiki moja baada ya jaribio la kumuuwa mmojawapo wa wanaharakati wake wakuu kulikofanywa na mwanaume wa Kipalestina na kupelekea Israel kulifunga eneo hilo ambalo ni takatifu kwa Waislamu halikadhalika kwa Wayahudi.

Msemaji wa polisi Luba Samri amesema waandamanaji kadhaa waliojifunika nyuso waliwarushia mawe na fataki vikosi vya usalama ambavyo baadae viliingia katika eneo la msikiti huo wa Al-Aqsa na kuwatimua waandamanaji hadi ndani ya msikiti huo.

Polisi yaingia msikitini

Msikiti wa Al-Aqsa ulioko Jerusalem.Picha: AFP/Getty Images

Katika hatua isio ya kawaida polisi iliingia mita kadhaa ndani ya msikiti kuondowa vizuizi vilivyowekwa na waandamanaji ili kujifungia ndani jambo ambalo msemaji huyo wa polisi amesema sio mara ya kwanza kufanyika.

Mapambano hayo yamezuka kutokana na waandamanaji wa Kipalestina kuwarushia mawe na fataki polisi baada ya kufunguliwa kwa Lango la Mughrabi kwa ajili ya watu wanaozuru eneo hilo.

Msemaji huyo wa polisi wa Israel ameendelea kufafanuwa kwamba kutokana na makabiliano kuwa mabaya na vitendo hivyo vya fujo vya Wapalestina, kwa lengo la kuzuwiya madhara dhidi ya polisi na kuondowa vizuizi vilivyowekwa mbele ya milango na uwanja wa eneo hilo takatifu polisi iliingia ndani mita kadhaa na kuweza kufunga milango ya msikiti huo wakati waandamanaji wakiwa ndani ya msikiti.

Inaelezwa kuwa hata hivyo eneo hilo baadae lilifunguliwa ili watu waweze kuendelea na ziara yao juu ya kwamba waandamanaji walikuwa bado wamefungiwa ndani ya msikiti huo.

Mapambano yazagaa

Mapambano kati ya polisi na Wapalestina yalizagaa kwa haraka na kuingia katika vichochoro vya mji wa kale wa Jerusalem.

Mojawapo ya vurugu kati ya polisi ya Israel na Wapalestina Jerusalem ya mashariki.Picha: Reuters

Karibu na Lango la Simba mojawapo ya milango saba ya kuingilia katika mji huo wa kale wa Jerusalem uliozungukwa na ukuta, polisi ya Israel ilifyatuwa gesi ya kutowa machozi na mabomu ya kutowa onyo kuutawanya umma mkubwa wa Wapalestina wenye hasira.

Omar Alkeswami meneja wa Kipalestina wa msikiti wa Al-Aqsa amesema watu 20 wamejeruhiwa katika purukushani hiyo ambayo pia imewakumba watoto kadhaa waliokuwa njiani kwenda shule wakati huo.

Mapambano hayo yamekuja wakati hali ya mvutano ikiongezeka kutokana na madai ya wafuasi wa sera kali wa Kiyahudi kutaka waruhusiwe kufanya ibada ndani ya eneo la msikiti huo na kutanuka kwa ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo la Waarabu la Jerusalem ya mashariki linalokaliwa kwa mabavu na Israel.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW