1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano Yemen yahatarisha juhudi za amani

Josephat Charo
26 Septemba 2023

Pande mbili katika mzozo uliodumu miaka minane nchini Yemen, waasi wa Houthi na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, wametuhumiana kwa mashambulizi yanayovunja hali ya utulivu na kuhatarisha mazungumzo ya amani.

Jemen | Kämpfer gegen die Huthi-Rebellen nahe Marib
Picha: Nariman El-Mofty/AP Photo/picture alliance

Mapambano yanayojitokeza nchini Yemen yanahatarisha juhudu za amani katika nchi ambako waasi wa Houthi wamekuwa wakipambana na muungano unaongozwa na Saudi Arabia tangu 2005, katika mzozo ambao umesababisha vifo vya maalfu ya watu na kuwaacha asilimia 80 ya wakazi wakitegemea msaada.

Msemaji wa Wahouthi Mohammed Abdulsalam amesema muungano huo uliwaua wanajeshi wake 12 mwezi uliopita kwenye eneo la mpaka na Saudi Arabia. Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran walikuwa wakijibu tuhuma za kuwaua wanajeshi wawili wa Bahrain na kuwajeruhi wengine kadhaa jana Jumatatu kwenye shambulizi la ndege isiyo na rubani katika mpaka wa kusini wa Saudi Arabia.

Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umelaani mauaji hayo na kusema yalifuatia mashambulizi kadhaa ya Wahouthi kwenye kituo cha kusambaza umeme na kituo cha jeshi la polisi karibu na mpakani.

Kamandi ya jeshi la Bahrain inasema mmoja wa maafisa wake pamoja na mwanajeshi mmoja waliuliwa kwenye shambulizi la ndege isiyo rubani na waasi wa Yemen waliokuwa wanapiga doria katika mpaka kati ya Yemen na Saudi Arabia. Taarifa ya jeshi la Bahrain iliyoripotiwa na shirika rasmi la habari la Bahrain inasema wanajeshi kadhaa walijeruhiwa katika shambuli hilo la mapema Jumatatu.

Taarifa hiyo ya jeshi pia imesema shambulizi hilo la kigaidi lilifanywa na waasi wa Houthi ambao walitumia ndege isiyo rubani kulilenga eneo la walinzi wa Bahrain katika mpaka wa kusini na ufalme wa Saudi Arabia licha ya kusitishwa kwa operesheni za kijeshi kati ya pande zinazohasimiana nchini Yemen.

Yemen imekabiliwa na machafuko yaliyowatumbukiza raia katika hali ya kutegemea misaadaPicha: picture-alliance/dpa

Saudi Arabia yalaani shambulizi

Saudi Arabia imelaani shambulizi hilo katika himaya yake lililowaua wanajeshi wawili wa Bahrain karibu na mpaka wake na Yemen. Wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia imetoa taarifa ya kulaani na kushutumu kile ilichokieleza kuwa ni shambulizi la kihaini dhidi ya Ufalme wa Bahrain upande wa mpaka wa kusini, ambalo lilisababisha kuuliwa kwa wanajeshi wake kadhaa na wengine kujeruhiwa.

Soma pia: Bahrain yasema wanajeshi wake wameuwawa na wengine kujeruhiwa

Taarifa ya Saudi Arabia haikuwalaumu moja kwa moja waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran, lakini ikarudia wito wa ufalme huo kutaka usafirishaji na upelekaji silaha kwa wahouthi ukome. Wahouthi hawajatoa kauli yoyote kuhusu shambulizi hilo.

Jana Jumatatu televisheni ya Wahouthi ya Al-Masirah iliripoti kwamba raia wanne walijeruhiwa katika mashambulizi ya Saudi Arabia katika himaya ya Yemen karibu na mpakani.

Shambulizi lililowaua wanajeshi wa Bahrain limefanyika wakati Saudi Arabia ikifanya juhudi kutafuta usitishwaji  mapigano wa kudumu, karibu mwaka mmoja na nusu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano na Wahouthi ambayo kwa kiwango kikubwa yameheshimiwa licha ya kufikia mwisho rasmi mwezi Oktoba mwaka uliopita.

(afp, rtre)