Mapambano ya rushwa yaporomoka katika nchi za Magharibi
10 Februari 2026
Ripoti hiyo imeeleza kuwa mataifa yaliyoimarika kidemokrasia duniani yanazidi kuporomoka katika maswala ya kupambana na ufisadi. kwenye Faharasi iliyochapishwa siku ya Jumanne, inaonyesha nchi za Magharibi zinakabiliwa na mmomonyoko kwenye maswala ya kupambana na ufisadi katika ngazi ya uongozi.
Toleo la 31 la Faharasi ya shirika la Transparency International limeorodhesha zaidi ya nchi na maeneo 180 ambayo viwango vya ufisadi vinaonekana katika sekta za umma na kupungua kwa watendaji imara wa muda mrefu.
Idadi ya nchi zilizopata alama zaidi ya 80 ambazo hapo awali zilikuwa kipimo cha utawala bora imepungua kutoka nchi 12 muongo mmoja uliopita hadi nchi tano tu imesema ripoti hiyo.
Transparency International imesema Denmark inaongoza kwa kupata alama (89) kwa miaka minane mfululizo, ikifuatiwa kwa karibu na Finland kwa alama (88) na Singapore alama (84), shirika hilo hata hivyo limelaani juu ya kukosekana "uongozi wenye ujasiri" duniani kote, jambo ambalo shirika hilo limesema linadhoofisha juhudi za kukabiliana na ufisadi.
Shirika hilo la kupambana na rushwa limeonya kuhusu kuongezeka kwa ufisadi katika nchi zilizokomaa demokrasia duniani kote na limesema alama za Marekani zimeshuka hadi kufikia alama za chini kabisa kuwahi kutokea.
Faharasi ya Transparency International, ndicho kielelezo cha kupanga kila taifa kwa kipimo kutoka 0 (ikimaanisha rushwa imekithiri) hadi alama 100 (kuonesha ubora), imeonyesha kuwa Marekani imeshuka kwa alama 10 hadi alama 64, tofauti na ilivyokuwa mnamo mwaka 2016.
Shirika la Transparency International lenye makao yake makuu mjini Berlin nchini Ujerumani, pia limesema wastani wa alama za kimataifa umefikia kwenye kiwango kibaya zaidi katika muongo mmoja.
Katika nchi za Magharibi kiwango cha kupambana na ufisadi kimeshuka zaidi nchini Uingereza. Nchi hiyo imeshuka kwa alama 11 hadi kufikia alama 70, jambo ambalo Transparency International imesema limetokana na kushindwa kudhibiti viwango vya maadili kwa mawaziri, wabunge na maafisa wengine wa serikali.
Mataifa mengine ya Magharibi yaliyoshuhudia kushuka kwa viwango vya kupambana na rushwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ni New Zealand, iliyoshuka kwa pointi tisa hadi 81, Sweden, ilishuka kwa alama 8 hadi kuwa na alama 80 na Canada ilishuka kwa pointi 7 hadi kufikia alama 75.
Ujerumani katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ilishuka kwa alama 4 hadi kuwa na alama 77. Mnamo mwaka jana nchi hiyo ilipanda kwa alama 2.