1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yaendelea Sudan licha ya juhudi za usuluhishi

Angela Mdungu
7 Mei 2023

Pande mbili hasimu zinaendelea na mapigano katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum pamoja na Darfur wakati ambapo jeshi la serikali na kikosi cha dharura cha RSF wamewatuma wawakilishi wao katika mazungumzo ya usuluhishi

Krieg in Sudan | Kämpfe in Khartoum
Picha: MOHAMED NURELDIN ABDALLAH/REUTERS

Mazungumzo hayo yanafanyika kwenye mji wa bandari wa Jeddah nchini Saudi Arabia wakati mapambano kati ya pande hizo mbili yakiingia katika wiki ya nne.

Majadiliano kati ya makundi hayo mawili yanayozozana yanasimamiwa na Marekani na Saudi Arabia kwa lengo la kupata makubaliano ya kudumu ya kusitisha vita. Makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa tangu Aprili 15 yalipoanza mapambano yamekuwa yakikiukwa.

Jenerali Abdel Fattah al-BurhanPicha: ASHRAF SHAZLY/AFP/Getty Images

Mazungumzo mengine yaliyopangwa kujadili hali ya mgogoro wa Sudan yanafanywa pia na muungano wa nchi za Kiarabu mjini Cairo Jumapili hii. 

Mapigano makali nchini Sudan tayari yamekwishasababisha mauaji ya takribani watu 700 wengi wao wakiwa ni raia. Maelfu ya watu pia wamejeruhiwa. Zaidi ya watu 100,000 wakiwem raia wa kigeni na wa Sudan wanaripotiwa kuwa wamelazimikia kulikimbia taifa hilo kutokana na machafuko.

Matumaini madogo ya kumaliza vita licha ya mazungumzo 

Licha ya kuwa pande mbili zinazokinzana zilikubali kushiriki mazungumzo yanayofanyika Saudi Arabia, zimekuwa zikisisitiza mara kadhaa kuwa zilikubaliana kuweka chini silaha ili tu kuruhusu misaada ya kiutu na siyo kukomesha mapambano.

Jenerali Mohamed Hamdan DagaloPicha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Kiongozi wa kikosi cha dharura cha RSF, Mohammed Hamdan Dagalo siku ya Jumamosi,  alithibitisha ushiriki wa kundi lake kwenye mazungumzo hayo ya Saudia. Alisema anatumaini kuwa watatimiza kusudi lao la "kusitisha vita, kuruhusu njia za kupitishia misaada ya kiutu na kutoa huduma muhimu kwa watu wa Sudan”

Dagalo Pamoja na Jenerali wa Jeshi la Sudan Abdel-Fattah Burhan wameapa kuendelea na mapigano hadi hatua ya mwisho.

Andreas Krieg wa chuo cha King cha mjini London, Uingereza aliliambia shirika la AFP kuwa, mapambano ya mjini Khartoum yanaelekea kwa haraka kuwa vita ya uasi ambapo pande zote mbili katika mzozo huo zina "uwezo na nguvu zinazofanana".