Mapambano yanaendelea kuudhibiti Kobane
10 Oktoba 2014Wajumbe wawili wa ngazi ya juu wa Marekani wamekutana jana na viongozi wa Uturuki wakitafuta kuishawishi nchi hiyo ambayo ni mshirika wake katika jumuiya ya NATO kuunga mkono mapambano ya angani dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, ambalo limekamata maeneo makubwa ya ardhi nchini Iraq na Syria.
Licha ya kwamba msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Jen Psaki hakuainisha majukumu maalum yaliyotolewa na Uturuki , amesema nchi hizo mbili zimekuwa na mazungumzo ya kina na yenye maelewano.
Marekani imeitaka Uturuki jana kujiunga na mapigano dhidi ya wapiganaji wa kundi la IS ambaol wanasonga mbele, ambao wamekamata sehemu ya mji muhimu wa mpaka na Syria wa Kobane licha ya mashambulizi ya anga yanayoongozwa na jeshi la Marekani.
Katika mapigano hayo ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya raia , miito imeongezeka ya kutaka majeshi ya ardhini kuwasaidia wapiganaji wa Kikurdi ambao wamezingirwa katika mji huo wa Kobane.
Uturuki yakataa kuchukua hatua pekee
Lakini baada ya mazungumzo na katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg , waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavosoglu amesema serikali ya nchi yake haiwezi kutarajiwa kuchukua hatua pekee.
Kobane mji ambao wanamgambo wa Kikurdi bado wanapambana baada ya mapambano ya wiki tatu sasa dhidi ya wapiganaji wa Jihadi, umekuwa eneo muhimu la mapambano katika vita dhidi ya kundi la IS. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema
"Kobane ni msiba kwasababu unawakilisha uovu wa kundi la IS lakini sio tafsiri ama ya maafa ama kiwango kamili cha yale yanayotokea kutokana na mapambano na IS. Ni mji mmoja na kutakuwa na mingine ambako kutakuwa na mzozo na IS katika muda wa miezi ijayo."
Afisa wa Kikurdi na wanaharakati wa Syria wamesema kundi la Dola la Kiislamu limeshambulia kwa makombora kituo cha mpakani kati ya Syria na Uturuki leo kujaribu kukikamata na kukata mawasiliano na mji wenye mapigano wa Kobane
Baadhi ya wadadisi wa masuala ya kijeshi wanafikiria kwamba majeshi ya Marekani yangepeleka ndege zaidi za upelelezi katika eneo la Kobane, na kuwezesha kutambua maeneo muhimu ya kushambulia. Lakini maafisa wa Marekani wamekataa kusema lolote kuhusu uwezekano huo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri:Yusuf Saumu