Mapambano yaongezeka Jerusalem
23 Julai 2017Wizara ya afya ya Palestina imesema Mpalestina mmoja ameuwawa katika mapambano tofauti nje ya mji huo, na kufikisha idadi ya watu waliouwawa katika muda wa siku mbili zilizopita kuwa saba. Hata hivyo wizara hiyo haikutoa maelezo zaidi ya vipi mtu huyo alifariki.
Waisraeli wawili walichomwa visu na kufariki siku ya Ijumaa wakati wakila chakula cha jioni katika makaazi ya Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi.
Masaa kadhaa mapema, Wapalestina wawili waliuwawa katika ghasia zilizozushwa kutokana na Israel kuweka vifaa vya ukaguzi katika eneo la kuingilia katika eneo hilo takatifu katika mji mkongwe uliozungushiwa ukuta.
Urusi, Marekani , Umoja wa Ulaya na Umoja wa mataifa , kile kinachofahamika kwa jina la pande nne za upatanishi wa amani katika mashariki ya kati , wamesema katika taarifa ya pamoja kwamba "wana wasi wasi mkubwa kutokana na hali ya wasi wasi inayoongezeka na ghasia na mapambano yanayotokea ndani na kuzunguka mji mkongwe wa Jerusalem", na kutoa wito wa kujizuwia kwa pande zote mbili.
Baraza la Usalama kujadili hali ya vurugu
Wanadiplomasia wamesema baraza la Usalama la Umoja wa mataifa litakutana kujadili hali hiyo Jumatatu. Sweden , Misri na Ufaransa zimeomba mkutano huo "kujadili kwa haraka vipi miito ya kupunguza hali ya wasi wasi mjini Jerusalem inaweza kuungwa mkono", mratibu wa baraza la usalama la Sweden , Carl Skau, aliandika katika ukurasa wa Twitter.
Rais wa palestina Mahmoud Abbas ameamuru kusitishwa kwa mahusiano yote rasmi na Israel hadi pale Israel itakapoondoa vifaa hivyo vya ukaguzi vya kugundua vitu vya cuma katika eneo hilo takatifu mjini jerusalem, mahali ambapo Waislamu wanasali katika msikiti wa al-Aqsa. Hakutoa maelezo zaidi, lakini mahusiano ya hivi sasa ni kwa kiwango cha chini katika ushirikiano wa kiusalama.
Baraza la mawaziri linalohusika na usalama la Israel linatarajiwa kuketi leo Jumapili (23.07.2017) na linatarajiwa kujadili hatua mbadala za kiusalama ambazo zinaweza kutumika badala ya vifaa hivyo vya kugundua vitu vya chuma, kwa mujibu wa maafisa wawili wa Israel , ambao wameomba majina yao kutotajwa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Sudi Mnette