1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yazuka kati ya majeshi ya Armenia na Azerbaijan

Sekione Kitojo
27 Septemba 2020

Mapigano yalizuka  kati  ya  Armenia  na  Azerbaijan leo katika eneo tete la Nagorno-Karabakh, na kufufua  wasi wasi wa kutokuwa na uthabiti katika eneo la kusini mwa Ulaya la Caucasus.

Aserbaidschan Berg-Karabach Militärkonflikt
Picha: Armenian Defense Ministry/AP/picture alliance

Eneo hili linapitia mabomba yanayosafirisha  mafuta na  gesi kwenda  katika masoko ya dunia.

Pande zote mbili, ambazo zimepigana  vita  katika  miaka  ya  1990, zimeripoti  watu kuuwawa. Armenia  na  Nagorno-Karabakh, jimbo linalotaka  kujitenga ambalo liko  ndani  ya  Azerbaijan lakini linaongozwa  na  watu  wenye  asili  ya  Armenia, ilitangaza  amri  ya kijeshi  na  kuwaita pamoja  raia  wake wote wanaume wa eneo  hilo.

Wanajeshi wa ulinzi wa Nagorno-Karabakh wakipata chakula huku wakilinda mipaka ya jimbo laoPicha: Karen Minasyan/AFP

Armenia  ilisema  Azerbaijan  ilifanya  shambulio  la  anga  na makombora dhidi  ya  Nagorno Karabakh. Arzebaijan ilisema  ilijibu mashambulizi  ya  makombora  ya  Armenia na  kwamba imechukua udhibiti  wa  zaidi  ya  vijiji  saba, lakini Nagorno Karabakh ilikana hayo.

Mapambano yamesababisha wimbi  la  hatua  za  kidiplomasia kuzuwia kuzuka  upya  kwa  mzozo  huo  wa  miongo  kadhaa  kati ya Waarmenia  ambayo  ina  wakaazi  wengi  Wakristo na  Azerbaijan ambayo  ina  Waislamu  wengi,  wakati  Urusi  ikitoa  wito  wa kusitishwa  mapigano  mara  moja  na kiongozi  wa  kanisa  Katoliki papa  Francis  akiongoza  miito ya   kufanyika  mazungumzo.

Gesi na  mafuta

Mabomba yanayosafirisha  mafuta  na  gesi katika  bahari  ya Caspian kutoka  Azerbaijan kwenda  katika  masoko  ya  dunia yanapitia  katika  eneo  hilo karibu  na  Nagorno - Karabakh. Armenia pia  imeonya  juu  ya  kitisho  cha  usalama  katika  eneo  la  kusini la  caucasus mwezi  Julai  baada  ya  Azerbaijan  kutishia kuwa  kuna uwezekano wa  kulipiza  kisasi kwa  kushambulia  kituo  cha kinyuklia  cha  nishati  cha  Armenia.

Nagorno-Karabakh , ilijitenga  kutoka  Azerbaijan  katika  mzozo ambao  ulizuka  wakati  Umoja  wa  Kisovieti ukisambaratika mwaka 1991.

Eneo la Nagorno-Karabakh Picha: Zuma/imago images

Licha  ya  kwamba  makubaliano  ya  kusitisjaji  mapigano  ulifikiwa mnao  mwaka  1994, baada  ya  maelfu ya  watu kuuwawa  na wengine  wengi  kukimbia  makaazi  yao, Azerbaijan na  Armenia mara kwa  mara  hushutumiana kwamba kuna  mashambulizi yamefanyika  karibu  na Nagorno-karabakh pamoja  na  eneo la mpaka  kati  ya  Azerbajain na Armenia.

Katika  mashambuliano  hayo  ya  Jumapili, wanaharakati  wa  haki za  binadamu  wa  Armenia walisema mwanamke  mmoja MmArmenia  na  mtoto wameuwawa. Aterbaijan ilisema  idadi isiyojulikana  ya  raia  wake wameuwawa. Nagorno - Karabakh imekana  ripoti  kuwa wanajeshi  wake  10 wameuwawa.

Ujerumani yataka mapambano kusitishwa

Waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Ujerumani  Heiko Maas  ametoa wito wa kusitishwa  mara  moja  mapigano  hayo katika  mzozo  huo unaojitokeza  tena  kati ya  Azerbaijan na  Armenia katika  jimbo  la Nagorno-Karabakh. Maas  ameelezea  wasi  wasi  wake  kuhusiana na  kurejea  kwa mapambano  makali kati ya  nchi  hizo  mbili.

Picha ikionesha kile jeshi la Armenia ilichosema kuwa ni gari lenye silaha za jeshi la Azerbaijan ambalo liliharibiwa na jeshi la Armenia leo tarehe 27.09.2020.Picha: Armenian Defense Ministry/Reuters

"Nazitaka  pande zote  katika  mzozo  huo kusitisha  mara moja mapigano  yote  na  hususan  mashambulizi  ya  makombora  dhidi ya  vijiji  na  miji," alisema, kwa  mujibu  wa  wizara  yake  mjini Berlin.

Rais Recep Tayyip Erdogan wa  Uturuki  ameihakikishia  Azerbaijan uungaji  mkono  wa  nchi  hiyo  katika  mzozo  na  Armenia katika eneo  la  nagorno-karabakh.

Erdogan aliandika  katika  ukurasa wa Twitter kwamba, "Taifa  la Uturuki, linasimama, kama ilivyo  kila  wakati, kwa uwezo  wake wote katika  upande  wa  ndugu  zao   wa  Azerbaijan.