1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapatano kati ya Israel na Hamas yaingia siku ya mwisho

27 Novemba 2023

Jumatatu ni siku ya mwisho ya makubaliano ya kusitisha mapigano katika Israel na Hamas, huku pande mbili zikionesha dhamira ya kurefusha mpango huo.

Hamas-Geisel Abigail Edan
Mmoja wa mateka watoto waliorejeshwa na Hamas.Picha: Ariel Schalit/AP/picture alliance

Makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na kundi la Hamas yameingia siku yake ya nne na ya mwisho leo Jumatatu huku wanamgambo hao wakisema wako tayari kurefusha utekelezaji wa makubaliano hayo baada ya kuwaachia huru mateka zaidi.

Miongoni mwa mateka 17 zaidi walioachiwa na Hamas, jana ni pamoja na mtoto yatima mwenye umri wa miaka 4 ambaye wazazi wake walikuwa miongoni mwa watu waliouwawa katika uvamizi wa Oktoba 7 uliofanywa na  Hamas dhidi ya Israel.

Soma pia: Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na Israel yanamaliza muda wake Jumatatu

Wapatanishi wa kimataifa akiwemo mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Joseph Borrell wanashinikiza usitishwaji mapigano uendelezwe.

Rais wa Marekani Joe Biden amesema anataraji makubaliano hayo ya muda mfupi yanaweza kuendelezwa mradi mateka wanaendelea kuachiwa huru.

Kundi la Hamas limesema ikiwa juhudi zitafanyika za kuwaachia Wapalestina zaidi walioko kwenye jela za Israel watakuwa tayari kuendelea kusitisha vita.