Mapigano Burundi yauwa 26
20 Aprili 2008Bujumbura :
Msemaji wa jeshi la Burundi amesema kwamba watu 26 wameuwawa katika mapigano kati ya waasi wa FNL na majeshi ya serikali, yalioingia siku ya tatu jana. Kanali Adolphe Manirakiza alisema waliouwawa ni wapiganaji 20 na wanajeshi 6 wa serikali, katika moja wapo ya mapigano makali mnamo miezi ya karibuni. Mapigano hayo yalianza Alhamisi usiku , huku wapiganaji wa FNL wakivishambulia vituo vya serikali katika vitongoji vya mji mkuu Bujumbura na wanajeshi kulazimika kujibu mashambulio.Hata hivyo akizungumza hapo mapema na Deutsche welle msemaji wa kundi hilo Pasteur Habimana, alidai ni majeshi ya serikali yanayowashambulia.Wasi wasi umezidi nchini humo tangu mwezi Julai mwaka jana, wakati waasi wa FNL walipojitaoa katika tume ya kisimamia usitishaji mapigano wakiwalaumu wapatanishi kwa upendeleo. FNL inaonekana kuwa ndiyo kikwazo cha mwisho katika kupatikana kwa amani ya kudumu nchini Burundi.