1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano dhidi ya Wanamgambo wa IS yapamba Moto

17 Oktoba 2014

Wapiganaji wa kikurdi wakisaidiwa na hujuma za ndege za kivita za nchi shirika zinazoongozwa wanaendelea kupambana na wanamgambo wa itikadi kali wa dola la kiislam katika mji wa Kobane wa Syria unaopakana na Uturuki.

Moshi unafuka Kobane na kuonekana hadi katika mji wa Uturuki wa MursitpinarPicha: Reuters/Kai Pfaffenbach

Mod:

Wapiganaji wa kikurdi wakisaidiwa na hujuma za ndege za kivita za nchi shirika zinazoongozwa na Marekani wanaendelea kupambana na wanamgambo wa itikadi kali wa dola la kiislam katika mji wa Kobane wa Syria unaopakana na Uturuki.Mizinga na mabomu yanaendelea kufyetuliwa na mapigano kupamba moto .Zaidi anasimulia Oummilkheir.

Atmo......

Hatima ya Kobane,mji wa tatu wanakoishi wakurd katika mpaka kati ya Syria na Uturuki,uliogeuka kitambulisho cha mpambano dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali wa Dola la kiislam-IS,haijulikani siku 30 tangu mapigano yaliporipuka.

Wanamgambo wa itikadi kali wanadhibiti "si chini ya asili mia 50 ya mji huo" kwa mujibu wa shirika la syria linalosimamia masuala ya haki za binaadamu,lakini wakurd kutokana na ushupavu wao na kusaidiwa na hujuma za madege ya kivita ya nchi shirika,wamefanikiwa kuwazuwia wasiendelee kusonga mbele tangu masaa 48 yaliyopita.

Wanajaribu kuwawekea mtego wanamgambo wa IS kwa kuendeleza mashambulio au kwa kujaribu kuqazingira katika makao makuu waliyoyateka ijumaa iliyopita" amesema mkurugenzi wa shirika hilo lenye makao yake nchini Uingereza Rami Abdel Rahmane na kuongeza hujuma za madege ya kimarekani zililenga mojawapo ya majengo hayo na kwamba mapigano yanaendelea.

Jana wanamgambo wa itikadi kali wa IS walifanya mashambulio karibu na kituo cha mpakani cha Uturuki huko Mursitpinar wakilenga kuifunga njia kati ya Kobane na Uturuki-ripota wa shirika la hbari la Ufaransa AFP amesema.

Jumla ya mizinga 16 ilifyetuliwa na wanamgambo wa IS hapo jana-shirika la haki za binaadam la Syria linasema.

Watu wasiopungua 662 wameuwawa katika kipindi cha mwezi mmoja wa mapigano ya kuwania mji wa Kobane.

Ili kuwasaidia wakurd,Washington inayoongoza ushirika dhidi ya IS imefanya zaidi ya hujuma mia moja tangu mwisho wa mwezi wa septemba dhidi ya vituo vya wanamgambo hao mjini Kobane..Zaidi ya hayo wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema maafisa wa Marekani wamekutana na wakurd wa chama cha Umoja wa kidemokrasia,akishadidia hata hivyo kwamba Washington haifikirii bado kuwapatia silaha na mafunzo wanamgambo wa kikurd.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry anasemekana anatafuta ushirikiano mkubwa zaidi na China na mataifa makubwa ya kiislam kusini mashariki ya Asia-Malaysia na Indonesia katika kampeni yao dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali wa dola la kiislam IS.Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa China Yang Jiechi anatarajiwa kuwasili Boston,anakotokea John Kerry leo hii,na badae waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani atakwenda Indonesia ambako atahudhuria sherehe za kuapishwa rais mpya Joko Widodo jumatatu ijayo.Mjini Jakarta waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani atakutana pia na waziri mkuu wa Malaysia Najib Razak.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW