1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Mapigano kati ya jeshi la Sudan na RSF bado kizungumkuti

5 Julai 2023

Mapambano makali ya vita yameripotiwa nchini Sudan, huku pia mashahidi wakiripoti juu ya kuangushwa kwa ndege moja ya kivita ya jeshi la Sudan, RSF yatajwa.

Sudan Soldaten der RSF Truppe
Wanamgambo wa kikosi cha msaada wa dharura nchini Sudan (RSF).Picha: Ashraf Shazly/AFP

Mzozo kati  ya jeshi la serikali ya Sudan na kikosi cha msaada wa dharura  cha RSF bado unaendelea kuididimiza nchi hiyo ambayo kwa zaidi ya miezi miwili bado inakabiliwa na vita vya makundi hayo mawili yanayowania madaraka. 

Soma zaidi:Mji wa Khartoum watikiswa na miripuko kwa mara nyingine

Kikosi cha RSF kinatajwa kuchukua udhibiti wa maeneo makubwa ya mji mkuu wa Khartoum  huku duru zikiarifu kuwa jeshi hilo sasa limeongeza wapiganaaji wa ziada kutoka Darfur na Kordofan ambao wanasambazwa katika miji  ya Omdurman , Bahri na Khartoum, miji mingine yenye makutano ya mto Nile ili kuongeza udhibiti wao.

Mashuhuda wa mapigano yaliyotokea jana huko wanasimulia kwamba mapigano hayo yalikuwa ni makali na kwamba jeshi la serikali lilikuwa likijaribu kuzuia kikosi cha RSF ambacho kilihitaji kukitwaaa moja ya kituo cha polisi.

Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo anayeongoza jeshi la msaada wa dharura la RSF.Picha: Umit Bektas/REUTERS

Soma zaidi:  Mapigano makali kati ya vikosi vya majenerali wanaohasimiana yautikisa mji wa Khartoum nchini Sudan

Mzozo huo uliibuka katikati mwa mabishano kuhusu mpango unaoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa wa kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia, miaka minne tangu kupinduliwa kwa aliyekuwa  mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir.

Kwa upande mwingine Mapigano makali pia yameripotiwa kutokea katika eneo zima la mji mkuu wa Sudan ambako mashahidi wameeleza  juu ya  kuangushwa kwa ndege moja ya kivita, huku mashambulio ya makombora na bunduki yakiyatikisa maeneo mengi yanayouzunguka mji huo.

Jenerali wa jeshi la Serikali ya Sudan Abdel Fattah al-Burhan.Picha: Sudanese Armed Forces/REUTERS

Chanzo kutoka kikosi cha wanamgambo cha RSF kimeeleza kwamba kundi hilo limehusika kuidungua ndege hiyo ya jeshi la serikali ya Sudan na Kikosi cha RSF kimesema kimemkamata rubani  baada ya kutuwa kwa mwavuli.

Wakati mapigano makali yakiendelea kushuhudiwa hasa katika mji mkuu wa  Khartoum na eneo la magharibi la Darfur, mamia ya raia walionaswa katika maeneo hayo wanatajwa kukosa huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji, chakula, dawa kwa karibu miezi mitatu sasa .
   
Kwa mujibu wa shirika lakimataifa la uhamiaji , hadi sasa takriban Wasudan milioni 2.2 wamekimbia makazi yao ndani ya nchi na zaidi ya watu laki sita wakivuka mipaka kutafuta sehemu zenye usalama. 
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW