1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano Kordofan kusini yawauwa watu 51

6 Machi 2026

Mapigano makali yanaendelea kushika kasi katika eneo la Kordofan kusini mwa Sudan, yakisababisha vifo vya makumi ya watu na kuzidisha mateso kwa raia.

Uharibifu uliofanywa katika kijiji na wanamgambo huko Sudan
Uharibifu uliofanywa katika kijiji na wanamgambo huko SudanPicha: AFP

Haya yanafanyika huku Umoja wa Mataifa ukionya juu ya kuongezeka kwa kiwango cha vurugu katika vita vinavyoendelea kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces – RSF.

Taarifa kutoka vyanzo vya kitabibu zinasema watuwasiopungua 51 wameuawa kati ya Jumatano na Alhamisi kufuatia mashambulizi na mapigano katika eneo hilo ambalo kwa sasa limekuwa uwanja mkali zaidi wa vita tangu mgogoro huo uanze Aprili mwaka 2023.

28 wauwawa na 60 kujeruhiwa

Katika mji wa Dilling uliopo katika jimbo la Kordofan kusini,wakazi wameripoti kushuhudia mashambulizi ya mizinga na droni kwa siku nzima ya Alhamisi, hali iliyosababisha uharibifu mkubwa wa makazi na miundombinu ya kiraia.

Wanamgambo wa RSF wakisherehekea ushindiPicha: REUTERS

Chanzo cha hospitali ya Dilling kimesema watu 28 wameuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo, wakiwemo wanawake na watoto.

 Wakazi wa eneo hilo wanasema mashambulizi hayo yamekuwa makali sana, huku mabomu yakidondoka tangu asubuhi na kusababisha nyumba nyingi kubomolewa.

 Wakati huo huo, jeshi la Sudan limetangaza kurejesha udhibiti wa mji wa Bara uliopo kwenye barabara muhimu inayounganisha mji mkuu Khartoum na mji wa El-Obeid, mji mkuu wa jimbo la Kordofan Kaskazini.

 Jeshi linasema kurejesha mji huo ni hatua muhimu katika kupunguza mashambulizi ya RSF dhidi ya mji wa El-Obeid, ambao kwa miezi kadhaa umekuwa ukilengwa na mashambulizi ya wanamgambo hao.

Hata hivyo, mashambulizi ya droni yameripotiwa kuendelea katika miji mbalimbali ikiwemo Kadugli na El-Obeid, huku mashambulizi yakilenga pia majengo ya serikali na hospitali. Katika hali ya kukimbia mapigano, maelfu ya wananchi wamelazimika kuhama makazi yao. Ruqaya al-Zaki, mkimbizi kutoka Sudan anaelezea masaibu yao.

"Hatuna chakula wala maji, hatuna hata nguo na tumekuja bila viatu, tumekimbia kwa miguu," alisema Ruqaya Al Zaki.

Vurugu zimeongezeka kwa kiwango cha kutisha

Akizungumzia hali hiyo, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema vurugu katika eneo la Kordofan zimeongezeka kwa kiwango cha kutisha, zikisababisha vifo na majeruhi kwa raia pamoja na kuharibu nyumba, hospitali na miundombinu muhimu.

Dujarric amesema mapigano kati ya RSF na jeshi la Sudan yameongezeka katika miji ya Dilling, Kadugli na El-Obeid, huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yakiripotiwa hata kulenga hospitali na kukatiza njia muhimu za usambazaji wa misaada.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane DujarricPicha: Bianca Otero/IMAGO

"Vurugu katika eneo la Kordofan nchini Sudan zimeongezeka, zikisababisha vifo na majeruhi kwa raia pamoja na uharibifu wa nyumba, hospitali na miundombinu muhimu, huku zikizuia upatikanaji wa misaada ya kibinadamu. Mapigano kati ya RSF na Jeshi la Sudan yameongezeka, mashambulizi ya droni yakiripotiwa katika miji ya Dilling, Kadugli na al-Obeid. Mashirika ya misaada yanaonya hali inazidi kuwa hatari na yanatoa wito wa kulindwa kwa raia na kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu," alisema Stephane Dujarric.

 Umoja wa Mataifa sasa umetoa wito kwa pande zote zinazohusika katika vita hivyo kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, kulinda raia na miundombinu ya kiraia pamoja na kuruhusu misaada ya kibinadamu kufika kwa usalama kwa wananchi wanaohitaji.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW