1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano makali yaendelea mashariki mwa Ukraine

21 Juni 2022

Maafisa wa Luhansk wamesema kuwa vikosi vya Urusi vimeingia katika eneo la viwanda la Sievierodonetsk baada ya kuanzisha mashambulizi makubwa.

Ukraine-Krieg | Erneute russische Offensive in Luhansk
Picha: REUTERS

Akizungumza Jumanne, Meya wa Mji wa Luhansk, Serhiy Haidai amesema mapigano yanaendelea katika eneo la mashariki wakati ambapo vikosi vya Urusi vinajipanga upya baada ya kuongeza shinikizo na kusonga mbele kwenye miji miwili. Haidai amesema kiwanda cha kemikali cha Azot ndiyo pekee katika eneo la Sievierodonetsk ambacho kinadhibitiwa na vikosi vya Ukraine.

Raia 300 wamejihifadhi Azot

Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine, Iryna Vereshchuk amesema kuna takribani raia 300 waliojihifadhi katika kiwanda hicho. Jana Ukraine ilikiri kwamba imepoteza udhibiti katika kitongoji cha Metiolkine kilicho katika eneo na Sievierodonetsk.

Ama kwa upande mwingine, Urusi imesema Wamarekani waliokamatwa nchini Ukraine walikuwa ni mamluki waliowapiga risasi askari wa Urusi na hawafungamani na mkataba wa Geneva.

Shirika la RIA limeripoti hayo Jumanne likimnukuu msemaji wa Ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov akisema Wamarekani hao wanapaswa kuwajibishwa kutokana na uhalifu walioufanya. Peskov amesema pia mchezaji wa mpira wa kikapu Mmarekani Brittney Griner, aliyekamatwa nchini Urusi tangu mwezi Februari, anakabiliwa na mashtaka ya jinai.

Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: Präsidentschaft der Ukraine/ZUMA/dpa/picture alliance

Huku hayo yakijiri Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Afrika imechukuliwa mateka katika uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, huku kukiwa na ongezeko la bei za vyakula. Matamshi hayo ameyatoa Jumatatu wakati akiwahutubia viongozi wa Umoja wa Afrika. ''Nawaalika kuizuru nchi yangu sasa ili kuangalia upya uhusiano kati yetu. Ninapendekeza kuanza kuandaa - kwa ombi letu la pamoja, mkutano mkubwa wa kisiasa na kiuchumi kati ya Ukraine na Afrika,'' alifafanua Zelensky.

Imechukua wiki kadhaa Zelensky kukubaliwa ombi lake la kuyahutubia mataifa ya Afrika, huku mengi yao yakiendeleza uhusiano wa karibu na Urusi na kushindwa kuunga mkono azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Afrika na uhusiano wake na Urusi 

Ukraine na mataifa ya Magharibi yana matumaini ya kudhoofisha uhusiano wa Urusi na Afrika kwa kusisitiza kwamba hatua ya Urusi ndiyo ya kulaumiwa kutokana na kusababisha uhaba wa ngano na mafuta ya kupikia pamoja na kupanda kwa bei ya chakula na petroli barani Afrika. Siku ya Jumatatu, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell alisema hatua ya Urusi kuzuia usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine ni uhalifu wa kivita.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Luxembourg Jean Asselborn, amesema Jumanne kuwa nchi za Ulaya zimeungana katika kuunga mkono kuipa Ukraine hadhi ya kuwa mwanachama mtarajiwa wa Umoja wa Ulaya. Amesema wanafanya kazi kujitahidi kufikia hatua ambayo watamwambia Rais wa Urusi, Vladmir Putin kwamba Ukraine ni ya Ulaya na watalinda maadili ambayo Ukraine inayapigania na kuyatetea.

(AFP, AP, Reuters, DW)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW