Mapigano makali yashuhudiwa mjini Hodeida, Yemen
19 Juni 2018Umoja wa falme za kiarabu umevisaidia vikosi vya serikali ya Yemen kupambana na kuingia uwanja wa ndege wa mji wa bandari wa Hodeidah na kuanza kushambulia katika shambulizi linalosemekana kuwa kali katika vita dhidi ya waasi wa Houthi vilivyodumu miaka mitatu nchini Yemen.
Umoja huo ulio na wanajeshi waliopokea mafunzo nchini Marekani umesema muungano umeingia uwanja wa ndege wa Hodeida ulio katika eneo la bahari nyekundu. Bandari ya mji huo wa Hodeida ni muhimu na inashughulikia asilimia 75 ya mauzo ya nje ya Yemen.
Anwar Gargash, Waziri wa Umoja wa falme za kiarabu anayehusika na mambo ya nchi za nje wa umoja huo, amesema miaka mitatu ya vita imekwisha na ni lazima waasi wa Houthi wafikirie umuhimu wa kutafuta suluhu la kisiasa.
Hata hivyo vita vya kung'ang'ania mji huo vimezua wasiwasi wa kutokea mgogoro mkubwa wa kiutu nchini humo ambayo tayari ipo katika hatari ya kukabiliwa na uhaba wa njaa.
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba shambulizi lolote katika bandari ya Hodeida linaweza kukwamisha usafirishaji wa msaada unaohitajika kwa watu milioni nane na laki nne nchini Yemen. Kwa sasa wakaazi wa eneo hilo wanaishi kwa hofu ya kutokea mashambulizi makali zaidi kutokana na mabasi na vifaru vya kivita kuonekana kuingia mjini humo.
Wakaazi wa mji wa Hodeida wanahofia mapigano kupamba moto mjini humo
Mkaazi mmoja ambaye hakutaka kutambulika akihofia kutiwa nguvuni, amesema wamepigwa marufuku kutumia simu za mkononi, kuchukua picha na wanahojiwa mara kwa mara kuhusu miendeno yao. Amesema waasi pia wameonekana kuanza kuchimba mahandaki. Mapigano mjini Hodeida yamesababisha familia 5,200 kukosa makaazi wakati vikosi vilivyotiifu kwa serikali vikionekana kusogea pwani ya bahari nyekundu.
Aidha muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ulianzisha operesheni kali wiki iliyopita iliyoitwa "Ushindi wa dhahabu" ulionuiwa kuwaondoa waasi mjini Hodeida, operesheni hiyo imesababisha mauaji ya wapiganaji 164 wengi wao wakiwa waasi hii ikiwa ni kulingana na taarifa kutoka kwa jeshi na wauguzi. mpaka sasa hakuna raia yeyote aliyethibitishwa kuuwawa katika operesheni hizo.
Tangu Saudi Arabia, Umoja wa falme za kiarabu na washirika wengine waliuingilia mgogoro wa Yemen mwaka 2015, kumekuwepo na duru kadhaa za mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa lakini yameshindwa kufikia suluhu la mgogoro huo.
Mjumbe maalum wa Umoja huo kwa ajili ya Yemen Martin Griffiths amekuwa na mazungumzo na waasi katika mji wanaoudhibiti wa Sanaa tangu siku ya Jumamosi ili kupata muafaka kutoka kwa viongozi wa waasi wa Houthi. Hata hivyo Mjumbe huyo ameondoka mjini humo hii leo asubuhi bila ya mafanikio yoyote.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo