1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano makali yazuka kati ya makundi hasimu mjini Tripoli

15 Agosti 2023

Mapigano makali kati ya makundi ya wanamgambo nchini Libya yamezuka katika mji mkuu Tripoli.

Wanajeshi wanaoegemea upande wa Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Libya Abdulhamid al-Dbeibah
Wanajeshi wanaoegemea upande wa Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Libya Abdulhamid al-DbeibahPicha: Hazem Ahmed/REUTERS

Wakaazi wa mji huo wamejikuta wamenaswa majumbani mwao kutokana na mapigano.

Wakaazi wa mji mkuu Tripoli wameshindwa kutoka nje kuyakimbia mapigano yaliyozuka usiku wa kuamkia leo, ambayo yanaonesha ndiyo mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa Tripoli mwaka huu.

Na taarifa za vyombo vya habari nchini Libya zinasema tayari watu wawili wameuwawa,na uwanja wa ndege wa Tripoli umeshafungwa.

Mapigano yalizuka usiku wa kuamkia leo kati ya kikundi cha wanamgambo cha 444 na kikosi maalum cha jeshi la Tripoli kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari ndani ya Libya.

Soma pia: Umoja wa Mataifa waonya utatuzi mkwako wa Libya

Mivutano iliizuka baada ya kudaiwa kwamba kiongozi wa kamandi ya 444 ameshikiliwa na kikosi kingine cha jeshi katika uwanja wa ndege mjini Tripoli.

Wizara ya afya imezitaka pande zote zinazopambana kuruhusu magari ya wagonjwa pamoja na timu za kutowa huduma ya dharura kuingia kwenye maeneo yenye waathirika,na hasa katika mji wa Kusini.

Lakini pia kuruhusu damu ipelekwe katika mahospitali ya karibu na mji huo. Bado haijafahamika wazi jumla ni watu wangapi waliouwawa.Shirika la hilali nyekundi nchini Libya halikupatikana haraka kuzungumzia hali ilivyo.

Shirika la OPS ambalo linahusika na sekta ya safari za ndege jana usiku lilisema kwamba ndege nyingi  ziliondoka katika uwanja wa ndege wa Tripoli kufuatia mapigano yaliyozuka huku ndege zilizokuwa zimepangwa kutuwa katika uwanja huo zikielekezwa kutuwa katika uwanja wa ndege wa karibu kwenye mji wa Misrata.

Kumekuwa na utulivu kwa miezi kadhaa Libya

Vita hivi vipya nchini Libya vimeongezeka baada ya kushuhudiwa miezi kadhaa ya utulivu katika taifa hilo, kufuatia takriban muongo mmkoja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Libya imekuwa katika vita muda mrefu vinavyohusisha serikali mbili zilizoingia kwenye  mkwamo wa kisiasa.Migawanyiko ya muda mrefu nchini humo imechochea mara nyingi matukio ya vurugu na machafuko katika mji mkuu Tripoli katika miaka ya hivi karibuni jambo machafuko hayo mengi yamekuwa yakidumu kwa saa chache tu.

Maandamano nje ya jengo la mashahidi mjini Tripoli kulalamikia juu ya hali mbaya ya kisiasa na ugumu wa maishaPicha: Mahmud Turkia/AFP

Lakini taarifa ya Ujumbe wa Umoja wa Umoja wa Mataifa wa kuisadia Libya iliyotolewa leo Jumanne,imeonesha Umoja huo unawasiwasi na matukio ya ukosefu wa usalama pamoja na mapigano hayo yaliyoanza  jana usiku.Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umetowa mwito wa kusitishwa mara moja machafuko hayo.

Soma pia: Halifa Haftar atoa kitishi kipya kuhusiana na mapato ya mafuta 

Na hata serikali zote mbili za Libya zinazohasimiana zimelaani mapigano yanayoendelea kupitia taarifa zao zilizotolewa nyakati tofauti hii leo. Bunge lililoko katika mji wa Mashariki wa Benghazi limesema utawala kinzani ulioko Tripoli  ndio unaowajibika na machafuko hayo.

Nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta iko kwenye mgawanyiko tangu mwaka 2014 zikiweko serikali mbili zinazokinzana moja ikiendesha shughuli zake Mashariki na nyingine ikijikita Magharibi,mjini Tripoli na zote kila mmoja inaungwa mkono na makundi yake ya wanamgambo yenye silaha pamoja na mataifa ya kigeni.

Na kwa ujumla Libya ilitumbukia katika vurugu na machafuko tangu mwaka 2011 pale lilipozuka vuguvugu lililoungwa mkono na jumuiya ya kujihami ya NATO, lililomuondowa madarakani na baadae kumuuwa kiongozi wa Muda mrefu Moammar Gaddhafi.